Wizara ya Ulinzi wa Umma ya Burundi imeamuru kukamatwa kwa mbunge maarufu wa upinzani, Pierre-Celestin Ndikumana kwa tuhuma za kupanga kumuua Rais Pierre Nkurunzinza na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Msemaji wa wizara hiyo, Pierre Nkurikiye, akizungumza jana wakati wa matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni, alisema kuwa mbunge huyo alibainika kuwashawishi na kuwapa mafunzo wafanyakazi wa nyumbani kwake ili watekeleze mauaji hayo.
Alisema kuwa Ndikumana aliwatayarisha wafanyakazi wake watatu na kuwapa mafunzo tangu mwaka 2015.
Nkurikiye aliongeza kuwa wafanyakazi hao wamekiri kupewa mafunzo na Ndikumana ili kufanya mauaji hayo, na wamekiri pia kuwa walipanga kuwaua wabunge ambao pia ni wanandoa wa chama tawala mwanzoni mwa Oktoba.
Kufuatia tuhuma hizo, chanzo cha kuaminika cha Bunge la nchi hiyo kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa taratibu za kumvua ubunge Ndikumana zitaanza punde.
Kwa upande wa Ndikumana, kabla hajaingia mikononi mwa polisi, amekaririwa na AFP akisema, “hizi tuhuma zimepikwa kwa lengo la kuniharibia kisiasa na kunitisha na kuninyamazisha”.