Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi ya Bunge wakishirikianana familia, wamekubaliana kuwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Marehemu Irene Alex Ndyamkama utapelekwa Bungeni Jijini Dodoma siku ya Jumatano Aprili 27, 2022 kwa ajili ya Ibada Maalum na Waheshimiwa Wabunge kutoa heshima zao za mwisho.
Baada ya Waheshimiwa Wabunge kutoa heshima zao za mwisho, mwili wa marehemu utapelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Siku ya Alhamisi tarehe 28 Aprili 2022 utasafirishwa kuelekea Sumbawanga, Mkoani Rukwa ambapo kutakuwa na shughuli ya kuaga mwili wa marehemu kwa utaratibu utakaoandaliwa na uongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi Mkoani hapo baada kuzikwa Aprili 29, 2022 Mkoani Katavi.
Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama aliyefariki siku ya Jumapili tarehe 24 Aprili 2022 katika Hospitali ya Tumbi Mkoani Pwani na Ofisi ya Bunge inaendelea kuratibu taratibu za mazishi kwa kushirikiana na familia ya Marehemu, taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.