Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Makete, Pasco Mgina ametoa kilio kwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) mkoa wa Njombe, Neema Mgaya juu cha changamoto ya kukosekana kwa uzio katika hospital hiyo hali inayotishia usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya.
Kilio hicho alikitoa wakati Mbunge huyo alipokwenda kutoa Msaada wa mashuka katika wodi ya kinamama na Watoto ambapo amesema kukosekana na uzio kunatarisha usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya.
“Kukosekana kwa uzio kumekuwa na mwingiliano wa wanyama kama Mbwa, Ng’ombe na Mbuzi ambao wamekuwa wakisambaza uchafu hali ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko pamoja na usalama” amesema Mgina.
Akizungumza mara baada ya kutoa misaada hiyo Mbunge viti maalumu, Neema Mgaya amesema changamoto hiyo ameichukua na kwamba serikali inayoongozwa na chama cha mapinduzi CCM imeweka mikakati thabiti ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
“Hii changamoto nimeichukua na mpango wa serikali ni kuhakikisha inaboresha huduma za afya ili wananchi ziwafikie kwa urahisi” amesema Neema Mgaya.
Mbunge huyo alitoa msaada wa Saruji mifuko 30 yenye thamani ya shilingi laki tano kwa gereza la wilaya ya Makete kwa ajili ya kujenga chumba cha matibabu cha kuhudumia wafungwa pia ametoa mifuko 30 wa ajili ya ujenzi wa ofisi ya umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Makete.
Naye Mkuu wa gereza la makete, Mrakibu Alois Kayera, amemshukuru mbunge huyo na kwamba aendelee na juhudi hizo za kutekeleza ilani kwa vitendo.
”kwa saruji hii hakika tumepata pa kuanzia, jeshi, wafungwa na mahabusu tuanakushukuru sana na uendelee na moyo huo huo” amesema Kayera.