Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) ametoa msaada wa vitanda vya kujifungulia katika jimbo linaloongozwa na Tundu Lissu (CHADEMA).
Amesema kuwa ametoa msaada huo mara baada ya kufuatwa na kuombwa msaada na siyo kisiasa kama inavyozungumzwa na watu wengine.
Kingu ameeleza kuwa katika jimbo linaloongozwa na Lissu wapo madiwani wanaotoka katika chama chake (CCM) na ndiyo waliomfuata kuomba msaada kwake na wala hakuwa na nia ya kufanya kazi ndani ya jimbo hilo bali ni moyo tu.
Amesema kuwa asingeweza kwenda kutoa misaada katika majimbo ya wana CCM kwa kuwa hawakumuomba na kama ikitokea siku wakahitaji msaada wake yupo tayari kuwasaidia kwa kadri ya uwezo wake.
“Mimi sioni ubaya. Watu wameomba msaada wa vitanda kwamba kina mama wanateseka. Marekani leo wanaisaidia Tanzania haina maana kwamba Marekani mambo yako supa. Lakini Marekani inatoa misaada ya mabilioni. Mimi kwenda kutoa msaada jimboni kwa Lissu haina maana kwangu nimemaliza changamoto za kwangu,” amesema Kingu
Hata hivyo, Katika hatua nyingine Kingu amesema anamuombe Lissu ambaye amemtaja kama Kaka yake apone ili aweze kurejea kwenye majukumu yake.