Mbunge wa Viti Maalumu kupitia chama cha mapinduzi CCM Manispaa ya Lindi, Hamida Abdala, ametoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mpilipili iliyopo Lindi Mjini.
 
Ametoa msaada wa viroba 3 vya unga, kiroba 1cha Sabuni, Maharage, Maziwa na Madaftari kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu ikiwa ni njia mojawapo ya kuwapa moyo wa kujiona wapo sawa na wanafunzi wengine na kuwapa moyo wa kupenda shule bila kujali mazingira wanayoishi.
 
Aidha Mbunge huyo amesikitishwa na uchakavu wa jengo linalotumiwa na wanafunzi hao na kusema atakutana na Mkurugenzi wa Manispaa waweze kuweka mazingira mazuri na kuahidi kuongeza madawati wanafunzi hao.
 
“Nasikitika kuona uchakavu wa darasa licha ya kuwa ni moja ambalo tumeshindwa kulisimamia na naahidi nitakutana na Mkurugenzi wa Manispaa ili tuweke katika hali nzuri na yenye usalama kwa maendeleo yenu kitaaluma,” amesema Mbunge huyo .
 
Ametaja changamoto nyingine ya upungufu wa madawati na ameahidi kuitatua na amewaomba viongozi wengine wawe na hali ya kutembelea mashule mbalimbali ili waweze kugundua changamoto zinazowakabili wanafunzi ili zitatuliwe na wanafunzi wapate matokeo mazuri kwenye mitihani yao.
 
Kwa upande wake mwl. Fadhili Saidi Mtitima ametoa pongezi kwa Mbunge wa viti maalumu kwa kuwapatia zawadi licha ya kusahaulika kwa kundi hilo lenye uhitaji maalumu na ametaja idadi ya wanafunzi hao jumla ni 32 huku wasichana wakiwa 10, wavulana 22 na hali ya kitaaluma wapo vizuri hivyo ameomba wazazi wawapeleke watoto wao wasiwafiche majumbani waende wakapate elimu yao ya msingi.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 24, 2019
Kauli zamponza Halima Mdee, adondokea mikononi mwa Polisi