Uongozi wa Klabu ya Mbeya Kwanza FC imemtangaza kocha wa zamani wa Dodoma Jiji, Mbwana Makata kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Makata anajiunga na Mbeya Kwanza FC baada ya kuondoka Dodoma jijini FC mwezi uliopita, huku nafasi yake ikijazwa na Kocha kutoka Burundi Masoud Djuma Irambona.
Uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu Jijini Mbeya, unaamini Kocha Makata ataweza kufanikisha mpango wa kukinusuru kikosi chao kisishuke Daraja, kufuatia hali kuwaendelea ndivyo sivyo hadi sasa.
Mbeya Kwanza FC ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 14 ilizozivuna katika michezo 18 iliyocheza hadi sasa.
Makata anachukua nafasi ya Kocha Maka Mwalwisi ambaye ataendelea na majukumu yake ya Mkurugenzi wa Ufundi katika klabu hiyo huku aliyekuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo Nizar Khalfan akijiunga na DTB FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ‘Championship’ kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo.