Aston Villa leo itakuwa na kibarua mbele ya Leicester City wakiwa nyumbani ikiwa ni mchezo wa Carabao ambapo timu hiyo inahitaji ushindi ili iweze kutinga hatua ya fainali.
Kocha mkuu wa Villa, Dean Smith amesema kuwa Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania anaweza kupata na nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza kwa siku ya leo.
Villa wanatakiwa kushinda mechi ya leo ili kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
Mbwana Samatta, nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania anayekipiga Klabu ya Aston Villa amesema kuwa kutua kwake ndani ya Aston Villa kutaungwa mkono na watanzania wengi watakaoishabikia timu hiyo.
“Ilikuwa ni maombi yangu ya muda mrefu na ndoto zangu kucheza Ligi Kuu ya England na tangu nikiwa mdogo nilikuwa nikiitazama ligi hii kwenye TV na Aston Villa ni miongoni mwa timu nilizokuwa nazitama. Kuja kwangu hapa ninaamini nitapewa sapoti na mashabiki wangu wa Tanzania,” amesema.
Mshambuliaji huyo ni mchezaji wa zamani wa timu ya African Lyon na Simba ndani za Tanzania na TP Mazembe ya Congo pia ni mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kusajiliwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu England.
Samatta amesaini mkataba wa miaka minne na nusu ndani ya Aston Villa akitokea Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.