Timu anayochezea nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta, KRC Genk ya Ubelgiji imepangwa kundi E katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya pamoja na mabingwa watetezi, Liverpool ya England, Napoli ya Italia na Salzburg ya Austria.

Katika droo ya michuano hiyo iliyofanyika sambamba na tuzo za Mwanasoka Bora Ulaya, Samatta amejikuta akiangushiwa kwenye kundi la mabingwa watetezi, Liverpool hivyo atakutana tena na Sadio Mane wa Senegal.

Mane aliiongoza Senegal kuichapa Tanzania ya Samatta 2-0 kwenye mechi ya Kundi C Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Juni mwaka huu nchini Misri.

Simba wa Teranga walifanikiwa kwenda hadi fainali, ambako walikutana tena na wapinzani wao wa Kundi A, Algeria na kuchapwa tena 1-0, bao pekee la Baghdad Bounedjah dakika ya pili tu Uwanja wa Kimataifa wa Cairo hivyo kulikosa taji la AFCON.

Kundi A linaundwa na PSG ya Ufaransa, Real Madrid ya Hispania, Club Brugge ya Ubelgiji na Galatasaray ya Uturuki, Kundi kuna B Bayern Munich ya Ujerumani, Tottenham Hotspur ya England, Olympiacos ya Ugiriki na Red Star Belgrade ya Serbia.

Kundi C linaundwa na Manchester City ya England, Shakhtar Donetsk ya Ukraine, GNK Dinamo ya Croatia na Atalanta ya Italia, Kundi D linaundwa na Juventus ya Italia, Atletico Madrid ya Hispania, Bayer Leverkusen ya Ujerumani na Lokomotiv Moskow ya Urusi.

Kundi E Liverpool, Napoli, Salzburg na KRC Genk, Kundi F kuna Barcelona ya Hispania, Borussia Dortmund ya Ujerumani, Inter Milan ya Italia na Slavia Praha ya Jamhuri ya Czech.

Kundi G lina Zenit ya Urusi, Benfica ya Ureno, Lyon ya Ufaransa na RB Leipzig ya Ujerumani na Kundi H linazikutanisha Chelsea ya England, Ajax ya Uholanzi, Valencia ya Hispania na Lille ya Ufaransa.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Samatta kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kuisaidia Genk kutwaa ubingwa wa Ubelgiji msimu uliopita.

Hata hivyo, msimu uliopita Samatta alicheza michuano ya Europa League na timu yake, ambapo Genk ilitolewa hatua ya 32 bora na Slavia Prague ya Czech kwa kuchapwa 4-1 nyumbani baada ya sare ya 0-0 ugenini.

Kesi ya Ndege ya ATCL iliyozuiwa Afrika Kusini kuanza kusikilizwa
Van Dijk ang'ara tuzo za mwanasoka bora Ulaya