Mpiganaji wa MMA, Conor McGregor amekamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka ya unyang’anyi wa simu na uharibifu wa mali, Miami nchini Marekani.
McGregor alikamatwa jana asubuhi, baada ya mwanamme mmoja kumripoti kuwa alimkwapua simu yake ya mkononi alipokuwa akijaribu kumpiga picha nje ya hoteli, akaiharibu na kisha kutokomea nayo.
Ahmed Abdirzak, ambaye alikwapuliwa simu hiyo, amesema simu yake iliyoharibiwa ilikuwa na thamani ya $1,000.
Polisi walimkamata dakika chache baadaye na kumpeleka selo. Aliachiwa leo kwa dhamana na kutoa neno kwa mashabiki wake.
“Uvumilivu kwenye hii dunia ni kitu muhimu ninachoendelea kukifanyia kazi. Ninawapenda mashabiki wangu kweli,” McGregor ameandika kwenye Twitter.
Hili ni pigo lingine kwa mpiganaji huyo ambaye amemaliza adhabu ya kufanya kazi za kijamii hivi karibuni, kufuatia tukio la mwaka jana la kushambulia kwa viti gari lililokuwa limebeba wapiganaji wenzake.