Bingwa wa mapigano ya UFC, Conor McGregor anashtakiwa tena na mpiganaji mwenzake kwa madhara yaliyotokana na kitendo alichokifanya Aprili mwaka huu cha kushambulia gari lililokuwa na timu ya wapiganaji.

McGregor alirusha kiti kwenye kirisha la basi la wapiganaji hao wa UFC baada ya mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Brooklyn nchini Marekani, na kuwajeruhi baadhi.

Michael Chiesa (pichani), mpiganaji aliyekuwa kwenye gari hilo amefungua kesi akidai kuwa tukio hilo lilimpa majeraha usoni na kumsababishia matatizo ya kiakili pamoja na matatizo ya kifedha.

Alisema kuwa baada ya kupata majeraha, alilazimika kuahirisha kushiriki pambano lake katika UFC 223 lililokuwa lifanyike siku mbili baadaye.

Conor McGregor

Chiesa mwenye umri wa miaka 30, kupitia nyaraka zake za mashtaka ambazo zimeshuhudiwa na vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na BBC, amewashtaki pia wamiliki wa ukumbi wa Baclays Center na anadai fidia.

Amedai kuwa wamiliki wa ukumbi huo walishindwa kuweka ulinzi wa kutosha hali iliyompa nafasi McGregor kufanya fujo.

Ingawa hakutaja kwenye nyaraka hizo kiwango cha madai, BBC imeeleza kuwa ni takribani $25,000,

MacGregor alikwepa kwenda jela mwezi Julai baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kushambulia kwa lengo la kuumiza, ambapo  alipewa faini na kutakiwa kufanya kazi za kijamii.

Mbabe huyo amerejea tena kwenye mapambano ya UFC baada ya kujaribu ulingo wa masumbwi na kupoteza dhidi ya Floyd Mayweather, na sasa atapambana na Khabib Nurmagomedov, Oktoba 6 mwaka huu.

Forbes: Orodha ya wana hip hop walioingiza fedha nyingi zaidi 2017/18
Makamu wa Rais mgeni rasmi tamasha la Urithi Festival