Bingwa wa mapigano ya UFC, Conor McGregory ametamba kumpiga vibaya bingwa wa masumbwi wa dunia ambaye hajawahi kushindwa, Floyd Mayweather, katika pambano la masumbwi kati yao litakalofanyika Agosti 26 mwaka huu nchini Marekani.
Wababe hao ambao jana walishiriki mkutano na waandishi wa habari kwa lengo la kulitangaza pambano hilo, walipeana tambo uso kwa uso huku kila mmoja akidai atashinda kwa ‘Knock Out’ (kabla ya raundi 12 kukamilika).
“Nitahakikisha ninakupiga na hutavuka raundi ya nne,”alisema McGregory. “Hujawahi kukutana na pigano kamili kwa sababu masumbwi pekee ni kama robo ya pigano, sasa hadi raundi ya nne utakuwa hujitambui (unconscious),” alitamba.
McGregory pia alimrushia kijembe baba yake Mayweather, Mayweather Sr. kuwa amemuingiza mwanae kwenye matatizo kwa kumshauri vibaya kukubali pambano hilo.
Kwa upande wake Mayweather, alitamba kuwa atamsambaratisha McGregory kwenye pambano hilo huku akisisitiza kuwa atamchapa ‘Knock out’ na kwamba mwenyewe atachagua aangukie upande upi.
“Unachotakiwa kufanya wewe [McGregory] siku ya pambano uje halafu mengine uniachie nikuoneshe. Nitakuchakaza na wewe utaamua uangukie kwa upande gani, utangulize sura au mgongo,” alisema Mayweather.
Mayweather alisisitiza kuwa kwakuwa ana umri wa miaka 40, anafahamu fika kuwa hawezi kupigana kama alivyokuwa anaweza miaka miwili iliyopita lakini hata uwezo alionao sasa unatosha kumchakaza McGregory.