Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameruhusu kuanzishwa kwa mchakato wa kurejesha kumbukumbu na Vifaa vya Jadi na Utamaduni vinavyohusiana na Historia ya Tanzania akiwemo mjusi mkubwa aina ya Dinosaur aliyeko nchini Ujerumani, ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii nchini humo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu hoja ya Mbunge Riziki Lulida aliyetaka kujua lini Serikali ya Tanzania itanufaika na mapato yatokanayo na mjusi aina ya Dinosaur ambapo Ujerumani inapokea mapato ya takriban dola bilioni 3.8 kama faida inayotokana na maonyesho ya mjusi huyo.
Akijibu swali hilo, Kairuki amesema, “nikuhakikishie tayari kama Serikali kupitia mazungumzo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyafanya na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeir tunayo kamati ya kiserikali yenye taasisi zaidi ya nane ambayo itasimamia suala hili na baadae tutaendelea na majadiliano ambayo mheshimiwa Rais ametoa baraka zake.”
Aidha, ameongeza kuwa Serikali iko katika taratibu za kidiplomasia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili mazungumzo rasmi yaanze kuhusiana na ‘artifacts’ zote na vifaa vingine ambavyo ni kwa ajili ya kumbukumbu ya Tanzania.
Kwa upande wake Lulida alifafanua kuwa kutokana mapato inayopata Ujerumani kwa kumuonyesha mjusi huyo, Serikali ya Tanzania inaweza kupata gawio, ili iweze kuliendeleza eneo la Tendaguru Mkoani Lindi ambako mjusi huyo alichukuliwa.