Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa lengo la Serikali kuweka mkazo mkubwa kwenye ujenzi wa viwanda ni kuona vinatoa ajira nyingi kwa wanaanchi na kuzalisha bidhaa bora zinazoweza kushindana ngazi ya kimataifa.
Ameyasema hayo alipoungana na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela kutembelea Kiwanda cha Kuchakata Mpunga cha Mw Rice Millers Ltd kilichopo Kihonda Mkoani Morogoro.
“Tumeweka mkazo mkubwa kwenye ujenzi wa viwanda lengo lake ni kuona wananchi wanaweza kuajiriwa vilevile kwa Watanzia ambao hawaamini kwamba viwanda vyetu haviwezi kushinda kimataifa, kiwanda hiki bidhaa zake wanazozalisha ni bora na kwa asilimia kubwa wanauza nje,” Amesema Prof. Mkumbo.
Aidha, Prof. Mkumbo amesema Serikali itaendelea kuenzi na kutekeleza sera na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira mazuri kisera, kisheria, kanuni na miongozo kwa wafanyabiashara ili wafanye kazi zao kwa uhuru na usalama hatimaye wapate faida ili waweze kulipa kodi.
Kwa Upande wake, Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema kwa sasa nchini tunazalisha tani milioni 3 za mchele na tunatumia tani milioni 1.3 za mchele kwa maana hiyo tunajitosheleza na tuna ziada, ili tuweze kuuza hiyo ziada inabidi tuongeze ubora na njia ya kuongeza ubora ni kama hivi kiwanda kinavyochakata mpunga hadi kuufungasha vizuri na kuuza kwenye soko na ndani na nje.
Amesema kampuni ya Williner wameeleza kuwa wanataka kuongeza uwekezaji katika ukoboaji wa mpunga ili waweze kuongeza uwekezaji inabidi kuongeza uzalishaji wa mpunga na wamekubalia kuanzisha vituo wa mashamba darasa ya mfano kwa ajiri ya wakulima wa mpunga ili waweze kulima kilimo chenye tija.