Patrick Malo amerejeshwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Burkina Faso kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Afrika kusini utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

Malo mwenye umri wa miaka 25 ameitwa kikosini kuchukua nafasi ya beki wa klabu ya Le Havre Yacouba Coulibaly, ambaye hatoweza kucheza mchezo huo mjini Johannesburg kufuatia majeraha ya mguu yanayomkabili.

Malo aliitumikia Burkina Faso mwezi uliopita katika michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya Senegal, ambayo ilimalizika kwa matokeo ya sare huku kocha Paulo Duarte akimskhutumu kucheza chini ya kiwango, jambo ambalo lilimkera na kutangaza kujitoa kwenye timu hiyo.

“Kila mmoja wetu anafanya makosa‚ lakini kwa Malo alipindukia kufanya makosa yake.” Alisema  Duarte.

Duarte amesema alichukizwa na kitendo cha Malo kwenda moja kwa moja katika vyumba vya kubadilishia, baada ya kumtoa katika mchezo wa pili dhidi ya Senegal, badala ya kukaa na wenzake katika benchi.

Burkina Faso wanaongoza msimamo wa kundi D kwa point sita sambamba na Cape Verde ambao wanashika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa

Hata hivyo Senegal wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D wana nafasi kubwa ya kufuzu fainali za kombe la dunia, baada ya shirikisho la soka duniani FIFA kuamuru mchezo wao dhidi ya Afrika kusini kurudia.

Diamond asherehekea siku ya kuzaliwa Amana, asimamisha shughuli
Hugo Broos: Ninafanya kazi bila mkataba