Maamuzi ya Uongozi wa Azam FC kuachana na Kocha Abdihamid Moallin, yamemuibua Mchezaji wa zamani wa Simba SC Frank Kassanga ‘Bwalya’ kwa kutoa ushauri wa bure kwa Wachezaji na Uongozi wa klabu hiyo.
Azam FC jana Jumatatu (Agosti 29), ilitangaza hadharani kufikia makubaliano na Kocha Moallin ya kuvunja mkataba, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wake tangu kuanza kwa msimu huu 2022/23.
Kassanga ameutaka Uongozi pamoja na Wachezaji wa Azam FC kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wanajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mabingwa Watetezi Young Africans.
Amesema Wachezaji wa Azam FC wanapaswa kutambua umuhimu wa jukumu walilonalo kwa sasa, na waache kabisa mawazo ya maamuzi yaliyochukuliwa kati ya Uongozi na Kocha Moallin.
Kuhusu Uongozi wa Azam FC, Kassanga amesema unapaswa kuleta Kocha mwenye weledi mkubwa ambaye ataisaidia timu hiyo kufikia malengo yake msimu huu katika Michuano ya Ligi Kuu na Kimataifa.
“Itategemea wachezaji wana ari gani ya kupambana, ingawa ninaamini kwa kikosi walichokisajili kina uwezo wa kucheza katika mfumo wowote atakaokuja nao Kocha Mpya.”
“Wachezaji wanapaswa kufanya kazi yao, maamuzi yaliyofikiwa kati ya Uongozi na Kocha yanapaswa kubaki kama yalivyo, ili yasiathiri mwenendo wa timu ambayo kwa sasa ipo katika maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans.”
“Kama kusajili wamefanya usajili mzuri sana, hivyo wanachotakiwa kukifanya viongozi wa Azam FC ni kumsaka Kocha mwenye uwezo mkubwa na mwenye kufahamu namna ya kupambana katika Ligi ya ndani na Michuano ya Kimataifa.” amesema Kassanga
Kocha Moallin aliajiriwa Azam FC kama Kocha wa Kikosi cha Vijana, lakini kufukuzwa kwa Kocha George Lwandamina kulimfanya apandishwe kwenye kikosi cha wakubwa msimu uliopita 2021/22.
Kocha huyo kutoka nchini Marekani mwenye asili ya Somalia, aliiwezesha Azam FC kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika.