Kiungo wa Timu ya Taifa ya Algeria, Haris Belkabla ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kuonekana mtandaoni katika kipande cha video akishusha suruali na kuonesha sehemu ya makalio mbele ya wachezaji wenzake.
Belkebla ambaye anachezea klabu ya Stade Brestois ya Ufaransa alikuwa ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho cha Taifa kinachoshiriki michuoano ya AFCON. Video hiyo iliyosambaa imeripotiwa kuwa ilichukuliwa wakati wakiwa hotelini.
Nafasi ya Belkebla imechukuliwa na Mohamed Benkhemassa anayechezea klabu ya USM Alger.
Algeria hiyo imepangwa katika kundi C katika michuano hiyo itakayoanza mwezi huu nchini Misri na itachuana na Tanzania, Senegal na Kenya.
“Kocha Djamel Belmadi aliamua kumuondoa Belkebla kwenye kikosi cha Taifa kutokana na tukio hilo la utovu mkubwa wa nidhamu. Kocha amechukua uamuzi huo ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa na nidhamu,” Shirikisho la Mpira wa Miguu la Algeria limeeleza kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameomba radhi kwa wachezaji na taifa lake kwa ujumla kutokana na tukio hilo ambalo ameliita la aibu.
“Ninaomba radhi kwa watu wa Algeria. Sikuwa nafahamu niko mubashara kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo kitendo nilichokifanya hakikuwa sahihi,” amesema.
“Nimefanya kosa na nimelipa gharama. Imenivunja moyo wangu. Ninatumaini Algeria itashinda AFCON, lakini ndoto yangu imeishia hapa,” ameongeza.
Ingawa ilikuwa mara ya kwanza kuchezea timu hiyo ya Taifa, kiungo huyo amewahi kushiriki kwenye kikosi cha taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 23.