Mchumba wa mwandishi wa habari wa Saudia aliyeuawa, Jamal Khashoggi amesema kuwa amesusia mwaliko wa rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House kwa madai kuwa kiongozi huyo hajaonyesha nia ya kutaka kujua ukweli kuhusu mauaji hayo ya kikatili.
Hatice Cengiz amekiambia kituo kimoja cha Televisheni nchini Uturuki kwamba mwaliko huo unalenga kubadili maoni ya Wamarekani
Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul nchini Uturuki wiki tatu zilizopita, kifo chake kikigubikwa na utata mkubwa.
Aidha, serikali ya Saudi Arabia imekanusha madai ya kuhusishwa kwa familia ya kifalme katika mauaji hayo na badala yake imelaumu watu iliyowataja kuwa maajenti wakatili.
Hata hivyo, mchumba wake huyo amesema kuwa kama angejua kuwa maajenti wa Saudi Arabia wana mpango wa kumuua mchumba wake huyo asingemruhusu kwenda kwenye ubalozi huo wa Saudia Arabia nchini Uturuki.