Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema kuwa litawachukulia hatua kali wale wote wanaowanyanyasa waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Hayo yamesemwa hii leo jijini Dar es salaam na Katibu wa baraza hilo, Kajubi Mukajanga wakati wa siku ya kimataifa ya kupinga jinai dhidi ya waandishi wa habari ambapo amesema kuwa baraza hilo halilidhishwi na hali ya uhuru wa habari ulivyo kwa sasa.

Amesema kuwa hali inatokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi pamoja na upindishwaji wa sheria unaolenga kuwakandamiza waandishi wa habari.

Aidha, amesema kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kasi ya kufungiwa kwa magazeti imeongezeka, ambapo hadi sasa magazeti sita yamefungiwa huku baadhi ya waandishi wa habari wakishambuliwa hali inayozidi kuhatarisha usalama wao.

“Waziri hana mamlaka ya kulifungia gazeti isipokuwa kuzuia mauzui fulani ambayo yanaonekana kuwa ni ya kichochezi,”amesema Mukajanga

Hata hivyo, Mukajanga amewataka waandishi wa habari kuendelea kuripoti matukio mbalimbali ya unyanyasaji ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Omog apania kuvunja rekodi uwanja wa Sokoine
Rais Mugabe ataka hukumu ya kifo irudishwe