Aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee amesema ataendelea kuwa mwanachama wa hiyari wa Chama hicho licha ya Kamati kuu ya Chama hicho kutangaza kuwafuta uanachama yeye na wenzake 18.

Mdee ameeleza hayo leo Desemba 1, 2020 katika mkutano na waandishi wa habari  ambapo amesema, endapo Chama kitawakataza yeye na wenzake kwenda bungeni na kuwateua wengine basi wataridhia hilo.

“Tutakubali kuachia ubunge, inawezekana chama kikatutoa tusiende bungeni na wakaenda wengine, ila tangu vyama vingi vimeanza hakuna uchaguzi ambao umefanyika bila kuwepo malalamiko ya uchaguzi ila wabunge walienda,”amesema Mdee.

Mdee ameeleza kuwa yeye na wenzake 18 walipokea wito Novemba 25 uliowataka kuhudhuria Kamati Kuu Novemba 27, lakini walimuandikia Katibu wa Chama asogeze mbele tukio hilo kwa wiki mbili wakitaka muda usogezwe kwa kuwa Katiba ya Chama inaruhusu na mwanachama anatakiwa kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu ndani ya wiki mbili.

Mwishoni mwa juma lililopita, Kamati kuu ya CHADEMA ilitangaza kuwafuta uanachama Mdee na wenzake 18 walioapishwa na Spika Ndugai kama wabunge wa viti maalum baada ya chama hicho kusema kuwa hakikutuma majina yoyote kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kiongozi wa Tigray amtaka Abiy kuondoa majeshi
Sure Boy: Azam FC bado tupo kwenye mbio za ubigwa

Comments

comments