Kiwanda cha Muziki wa Tanzania kinaendelea kukua kwa kasi, na hilo linajidhihirisha kutokana na namna ambavyo wasanii mbali mbali wamekuwa wakifanya kazi ambazo mafanikio yake yamekuwa wazi hasa kupitia wingi wa idadi ya watu ambao wamekuwa wakifuatilia kazi hizo kupitia kwenye mifumo mbali mbali ya kusikilizia na kupakua muziki mtandaoni (Digital platforms).
Hizo ni miongoni mwa njia zinazotajwa kuwa sehemu kubwa ya mafanikio kwa wasanii kutokana na kuwaingizia kipato kwa urahisi zaidi ukiachana na kutumbuiza kwenye matamasha nk.
Zipo njia nyingi sana nyingine zikiwa za Kimataifa na Kitaifa vile vile ambazo wasanii huzitumia kuzipeleka kazi zao kwenye soko la muziki Duniani ambapo miongoni mwa mifumo hiyo ni pamoja na Mdundo Records.
Mdundo ni moja ya platforms kutoka nchini Tanzania iliyofanikiwa kuweka rekodi ya kufikia jumla ya wafuatiliaji milioni 16.4.
Hii inatajwa kuwa moja ya mifumo bora ya huduma za muziki mtandaoni ambayo imeweka rekodi ya kipekee Barani Afrika baada ya kufikisha idadi hiyo ndani kipindi cha robo tatu ya mwaka wa 2021, kilichoishia Septemba mwaka huu.
Matokeo hayo ni ongezeko la asilimia 10, ambapo ongezeko hilo limechangiwa na idadi kubwa ya watumiaji wapya kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Afrika Kusini jambo lenye kuendelea kuonyesha namna kiwanda cha Muziki kinavyo endelea kukua kwa kasi kuanzia ndani mpaka nje ya mipaka.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania iliongoza kwa kuwa na watumiaji wapya katika robo tatu ya mwaka ambapo jumla ya watumiaji wapya 4.1 waliripotiwa, huku Nigeria na Kenya zikirekodi watumiaji wapya milioni 3.1 na milioni 2.6.
Nchini Tanzania, Mdundo ilikua kwa asilimia 36 kutokana na watumiaji wapya milioni 4.1 hivyo kuchangia asilimia 24 ya jukwaa la watumiaji katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa 2021.
Hii inadhihirisha ukubwa na mafanikio ya tasnia kuanzia kwenye mapokezi ya kazi za wasanii kupitia Local digital platforms ambazo ni vyanzo vikubwa vya mafanikio yao.