Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya meatu, Athman Masasi ameongoza kikao Cha Kamati ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika ukumbi wa Halmashauri.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wa MTAKUWWA ngazi ya Wilaya ya Meatu chini ya mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Masasi
Pamoja na Wageni waalikwa kama Katibu Tawala wa Wilaya Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Eliasa Mtarawanje, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, wageni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wakiongozwa na Kamishna wa Kazi, Suzan Kangoni, pamoja na ugeni wa wawakilishi wa kutoka Shirika la kimataifa la Kazi ILO Kwa nchi za Afrika Mashariki pamoja na Brazil.
Mkutano huu ulishirikisha wawakilishi wa wakulima wa Pamba wilayani Meatu na Viongozi wa AMCOS.
Lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutambulisha Mradi wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watoto yaani utumikishaji watoto katika uzalishaji wa zao la Pamba, pamoja na kuinua uzalishaji wa zao la Pamba Meatu Kwa kizingatia ubora na staha katika kumlinda Mtoto wa Mkulima.
Mradi huu utatekelezwa na kuratibiwa kwa muda wa miaka miwili na utatekelezwa katika Wilaya ya Meatu pekee.
Aidha, imeelezwa kuwa sababu ya kuichagua Meatu ni kutokana na umahiri wake katika kupinga na Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watoto eneo ambalo Wilaya inafanya vizuri zaidi.
Pia Wilaya hiyo inafanya vizuri katika uzalishaji wa zao la Pamba.
Akiwasilisha mada ya ufunguzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri amesisitiza kuwa Halmashauri Iko tayari kutoa ushirikiano katika mradi huo.
“Kwa nafasi tulionayo sisi kama uongozi,naomba niwahakikishie tupo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali kwakuwa lengo letu ni moja ambalo ni kumsaidia mtoto kuondokana na unyanyasaji wa namna yoyote ile.” amesema Masasi.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Wilaya ya Meatu ndugu Eliasa Mtarawanje akimwakilisha Mkuu wa Wilaya alitumia fursa hiyo kuwashukuru Viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kwa kuichagua Meatu na kuona inafaa kutekeleza mradi huo na Kwamba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itatoa ushirikiano katika kila hatua ya mradi.
Wageni wamepata nafasi ya kutembelea eneo la Bibiti jineri kujionea uchakataji wa Pamba unavyofanyika.