Kikosi cha Kagera Sugar ndio kinayoburuza mkia kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa kikiwa hakina alama yoyote wala bao, licha ya kucheza michezo miwili, jambo hilo limemchefua kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Mexime aliyeamua kufuta mapumziko kwa wachezaji akitaka wajifue ili warudi kivingine ligi ikielendelea tena wiki mbili zijazo.
Timu hiyo ilianza kwa kupoteza mbele ya wageni wa ligi, Mashujaa mabao 2-0 kisha ikafungwa 1-0 na Ihefu na kuifanya iwe timu pekee isiyo na alama hata moja hadi sasa kati ya timu l6 zilizopo msimu huu na hali hiyo imemzindua Maxime na kuwaambia wachezaji hawatakuwa na mapumziko licha ya ligi kusimama.
Maxime amesema awali nyota hao walipaswa kupewa mapumziko ya siku nne hadi tano ila kwa sasa ratiba hiyo imefutwa ili kuendelea na programu mbalimbali za mazoezi ili kujiweka fiti zaidi.
“Hatujaanza vizuri msimu na sio jambo jema kwetu, hivyo tumeona tuendelee kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili ligi itakaporudi tena tuwe tumefanyika kazi upungufu uliojitokeza katika michezo iliyopita,” amesema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
Maxime ameongeza shida iliyopo ndani ya kikosi hicho ni kukosa utulivu kwenye maeneo mawili ambayo ni ulinzi na ushambuliaji.
Tumekuwa na maingizo mapya mengi, hivyo kikubwa hapa ni kutengeneza muunganiko kati yao na wale waliokuwepo mwanzoni, naamini kucheza ugenini michezo yote miwili ilitugharimu ila tunaangalia mbele kwa sasa,” amesema.
Ligi imesimama kwa muda wa majuma mawili kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa kwa timu za taifa na itarejea tena Septemba 15, Kagera itacheza siku inayofuata dhidi ya Geita Gold, Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba ukiwa ni wa kwanza nyumbani.