Klabu ya Kagera Sugar imepania kufanya vizuri katika msimu ujao baada ya kuendelea kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wawili wazoefu na mikikimikiki ya ligi kuu Tanzania bara.

Wachezaji hao ni golikipa Hussein Sharif ‘Cassilas’ na winga Ibrahim Twaha ‘Messi’ kwa ajili ya kuongeza kasi kwa Wanankurumbi hao ambao msimu uliopita hawakuwa katika ubora mzuri.

Kocha mpya wa timu hiyo Mecky Mexime amesema anaendelea kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wazuri ambao wataziba mapengo kulingana na mapungufu yaliyojitokeza msimu uliopita.

Hussein Sharif ‘Cassilas’

Ibrahim Twaha ‘Messi’

“Ni kweli tumewasajili Cassilas na Messi kwa ajili ya kuongeza nguvu ndani ya kikosi, tunaamini kutokana na uzoefu Ibrahim Twaha ‘Messi’ wao wa ligi watakuwa msaada mkubwa kwetu,” alisema Mexime.

Msimu uliopita kocha huyo pamoja na Cassilas walikuwa wakiwatumikia wakata miwa wa Mtibwa Sugar huku Messi akiwa na Wagosi wa kaya Coastal Union ambao wameshuka daraja na kuweka nia ya dhati ya kurejesha makali yaliyopotea katika siku za karibuni.

Nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na timu ya taifa Taifa Stars, alijiunga na wakata miwa wa mkoani Kagera hao mwanzoni mwa mwezi huu baada ya kutimuliwa Adolf Rishard aliyeweza kuinusuru na janga la kushuka daraja.

Kagera ni miongoni mwa timu zinazotoa upinzani wa kweli katika ligi kuu kwa misimu kadhaa iliyopita licha ya mwaka jana kupita katika wakati mgumu.

Prince Owusu: Naifahamu Vizuri Young Africans
Cristiano Ronaldo Aendelea Kutamba Duniani