Kocha Mkuu wa Kituo cha Kukuza Vipaji vya Soka cha Cambiasso, Mecky Maxime amesema Beki na Kiungo wa Young Africans Yannick Bangala Litombo, ana sifa zote za kuchukua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara Msimu huu 2021/22.
Mexime ambaye aliwahi kuvinoa vikosi vya Klabu ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar kwa nyakati tofauti, amesema amemfuatilia kwa muda Beki na kiungo huyo kutoka DR Congo na kubaini ana kipaji kikubwa, huku akiisadia sana Young Africans kusogelea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Amesema Bangala anajua sana kucheza soka kwa kufuata misingi yote ya uchezaji pindi timu ikiwa inashambuliwa ama kushambulia, na amedhihirisha hilo katika michezo yote aliopata nafasi ya kuitumikia klabu yake ya Young Africans.
“Niseme wazi kwangu katika kikosi cha Young Africans na hata waliopo katika Ligi Kuu Bara, Bangala ndiye mchezaji bora. Huu ni mtazamo wangu tu, lakini natambua wanaoshughulika na kazi ya kuamua wao wanajua zaidi ya hivyo nisinukuliwe vibaya,” amesema Maxime.
Bangala alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu huu 2021/22, akitokea FAR Rabatt ya Morocco.
Bangala pia aliwahi kucheza soka nchini kwao DR Congo kwenye klabu za DC Motema Pembe na AS Vita.