Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Mecky Mexime amesema sare ya 1-1 dhidi ya Simba SC ni kama ushindi kwa wachezaji wake kutokana na ugumu wa mchezo huo, uliopigwa jana Jumatano (Desemba 21) majira ya Usiku Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba-Kagera.
Kagera Sugar walitangulia kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Deus Bukenya dakika ya 15, kabla ya Simba SC kusawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Beki kutoka DR Congo Enock Inonga Baka dakika ya 39 Kipindi cha Kwanza.
Kocha Mexime amesema pamoja na kushindwa kupata alama tatu nyumbani, bado matokeo hayo ya sare sio mabaya kwa upande wake kwani imekua kipimo kizuri kwa Kagera Sugar, ambayo ilikabiliwa na michezo miwili mfululizo dhidi ya timu zenye uwezo mkubwa kisoka.
Amesema Wachezaji wake walipambana kwa kufuata maelekezo yake, lakini Simba SC walitumia uzoefu wao na kuwabana huku wakiwashambulia mara kwa mara na kufikia hatua ya kugawana alama.
“Hii kwangu mimi nimeshinda, Kocha unatakiwa ujipime kwa kucheza na timu kama hizi ambazo zipo vizuri na hata ukipata sare unatakiwa ujihesabu kama umeshinda, kwa hiyo mimi nawapongeza wachezaji wangu”
“Tumecheza hapa na Azam FC siku kadhaa zilizopita tumepata matokeo ya 2-2, kwa hiyo utaona wachezaji wangu wameonesha kupambana na kuzingatia ninachowaelekeza, kwa ujumla ulikua mchezo mzuri dhidi ya Simba SC, mchezo huu umekwisha tunajipanga na mchezo mwingine.” amesema Mexime
Kagera Sugar itacheza ugenini mwishoni mwa juma hili dhidi ya Geita Gold FC katika Uwanja wa Nyankumbu, huku wenyeji wao watarajiwa wakiwa na kumbukumbu ya kuambulia alama moja dhidi ya Azam FC kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 walioipata jana Jumatano (Desemba 21).
Simba SC inarejea jijini Mwanza kucheza mchezo wake wa Mzunguuko wa 18 dhidi ya KMC FC iliyouchagua Uwanja wa CCM Kirumba kama Uwanja wake wa nyumbani, ikitokea jijini Dar es salaam.