Kinara wa mabao katika ligi kuu ya soka Tanzania bara Meddie Kagere, amefunguka kuhusu usajili wa klabu yake ya Simba SC, ambayo inaongoza msimamo wa ligi hiyo.
Kagere ambaye kwa sasa yuko nchini kwao Rwanda alikojiweka mwenyewe karantini na familia yake ili kujiepusha na virusi vya Corona, amesema kwamba Simba kwa sasa ni timu kubwa ya kimataifa na yenye wachezaji bora, hivyo watakaokuja watapaswa kuwa bora zaidi ya waliopo yaani aliyepo ndani ya uwanja akimuangalia wa benchi atokwe na jasho.
“Wachezaji wote waliopo ni bora sana, ndio maana tunafanya vizuri mpaka sasa, hivyo viongozi wetu wanahitaji kutumia akili za ziada ili hao watakaokuja wawe mafundi zaidi, yaani namba moja iwe na wataalamu zaidi ya wawili, ili kikitoka kitu kinaingia kitu zaidi,” alisema mchezaji huyo raia wa Rwanda aliyezaliwa Uganda.
“Kama tunaongeza beki, basi anahitajika kuwa na uwezo zaidi ya waliokuwapo katika timu wakati huu. Yaani atakayeingia na atakayetoka pasiwe na tofauti.
“Tukifanikiwa kuingiza wapya wenye ubora kama au zaidi ya sisi tuliopo itaongeza hali ya kushindana na kila mmoja ataongeza umakini ili kupata nafasi ya kucheza, atataka kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika nafasi ambayo anaitumikia.
“Hii itasaidia kubadilisha ubora soka letu kwa vile ni klabu kubwa ya kimataifa, lengo letu wachezaji ni kutwaa vikombe mbalimbali zaidi ilivyo sasa, halitakuwa jambo la kupendeza kama wanasajiliwa wachezaji wapya ambao wanakuja katika timu wanaonekana tayari wamelewa mafanikio na kushindwa kutoa ushindani kwa ambao wamewakuta.”
“Hivyo ndivyo mtazamo wangu ulivyo, naona tutakuwa na kikosi bora na imara zaidi huku tuendako na mashabiki watafurahi,” aliongeza Kagere mwenye mabao 19 kwenye Ligi Kuu Bara. “Lakini jambo jingine ambalo litakuwa la kupendeza katika timu ni kuwe na wachezaji wengi wa viwango vya juu.
“Haitakiwi mchezaji fulani akikosekana katika mechi mashabiki au wachezaji wenyewe wasikitike, bali inatakiwa yeyote ambaye anakuwapo kazi ifanywe kwa ubora uleule au unaokaribiana. Huo ndio mtazamo wangu katika usajili wetu msimu huu”