Beki wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC Mehdi Benatia ametajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Morocco kitakachopambana na Cameroon, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika 2019, utakaochezwa Novemba 16.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Morocco Herve Renard, amemrejesha kikosini beki huyo, ambapo kwa mara ya mwisho alimtumia wakati wa fainali za kombe la dunia, zilizofanyika nchini Urusi kati kati ya mwaka huu.
Benatia mwenye umri wa miaka 31, amekosa michezo mitatu ya kuwania kufuzu fainali za Afika 2019, na aliamua kuelekeza mawazo yake katika kuisaidia Juventus FC, ambayo inatetea ubingwa nchini Italia.
Kwa sasa beki huyo anakabiliwa na upinznai mkubwa kwenye kikosi cha Juventus FC, baada ya kurejea kwa beki mzawa Leonardo Bonucci, aliyesajiliwa akitokea AC Milan wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.
Mpaka sasa Benatia ameshacheza michezo mitano pekee, akiwana kikosi cha Juventus katika michuano yote wanayoshiriki msimu huu.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa, ametaja kikosi cha wachezaji 26, ambacho kitakua na kazi kubwa ya kujiandaa kikamilifu kabla ya kuwakabili Cameroon, na kuhakikisha wanapata ushindi, utakaofanya kusubiri alama moja, ili kujihakikishia kufuzu kwa fainali za Afrika za mwakani.
Mchezaji mwingine aliyeitwa kwa mara ya kwanza baada ya fainali za kombe la dunia 2018, ni Sofiane Boufal wa klabu ya Celta Vigo ya Hispania.
Kwa mara ya mwisho Boufal aliichezea Morocco katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uzbekistan mwezi Februari, lakini alishindwa kumshawishi kocha kumjumuisha kwenye kikosi cha mwisho kilichokwenda Urusi kushiriki fainali za kombe la dunia.
Mpaka sasa Boufal ameshacheza michezo tisa ya ligi ya Hispania (La Liga) na amefunga mabao mawili.
Katika hatua nyingine kocha Renard amemuita kwa matra ya kwanza mchezaji Oussama Idrissi mzaliwa na Uholanzi, katika kikosi ambacho kitacheza mchezo dhidi ya Cameroon, na siku nne baadae kitapambana na Tunisia kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, aliwahi kuzitumikia timu za taifa za vijana za Uholanzi, lakini kwa kipindi kirefu ameshindwa kupata nafasi kwenye timu ya taifa ya wakubwa, hali iliyomfanya atafute mbinu za kulitumikia taifa lenye asili ya wazazi wake.
Kikosi kamili kilichotajwa kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika 2019, pamoja na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Tunisia.
Makipa: Munir El-Kajoui (Malaga, Spain), Yassine Bounou (Girona, Spain) na Ahmed Reda (Wydad Casablanca)
Mabeki: Medhi Benatia (Juventus. Italy), Nabil Dirar (Fenerbahce, Turkey), Manuel da Costa (Istanbul Basaksehir, Turkey), Romain Saïss (Wolverhampton Wanderers, England), Achraf Hakimi (Borussia Dortmund, Germany), Noussair Mazraoui (Ajax, Netherlands), Oualid El Hajjam (Amiens, France) na Achraf Dari (Wydad Casablanca)
Viungo: Hakim Ziyech (Ajax, Netherlands), Mbark Boussoufa (no club), Karim El Ahmadi (Al-Ittihad, Saudi Arabia), Younes Belhanda (Galatasaray, Turkey), Nordin Amrabat (Al Nassr, Saudi Arabia) na Faycal Fajr (Caen, France), Youssef Ait Bennasser (Monaco, France), Abdelilah Hafidi 30 (Raja Casablanca), Sofiane Boufal (Celta Vigo, Spain), Amine Harit (Schalke 04, Germany)
Washambuliaji: Oussama Idrissi (AZ Alkmaar, Netherlands), Khalid Boutaib (Yeni Malatyaspor, Turkey), Youssef En-Nesyri (Leganes, Spain), Ayoub El Kaabi (Hebei China Fortune, China) na Walid Azaro (Al Ahly, Egypt)