Uongozi wa Dodoma Jiji FC imemwongeza mkataba Kocha Kutoka Marekani Melis Medo na sasa ataendelea kuwepo mpaka mwishoni mwa msimu ujao.
Kocha huyo alijiunga na klabu hiyo Oktoba mwaka jana kuchukua nafasi ya Mrundi, Masoud Djuma ambaye alitimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema uongozi umeridhika na kazi ya kocha huyo na kuamua kumuongeza mkataba huo.
“Tumemwongeza mkataba Medo kwa sababu alivyokikuta kikosi ni tofauti na alivyokitengeza na kilivyomaliza ligi, kusema kweli sisi kama viongozi tulipambana na yeye mwenyewe aliinua viwango vya baadhi ya wachezaji na kuwarudishia morali wale wote waliokata tamaa, kwa hiyo tumempa nafasi nyingine msimu ujao,” amesema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Aidha, amesema Kocha huyo tayari amewasilisha ripoti yake ya msimu uliopita na wameanza kuufanyia kazi.
Dodoma Jiji ilimaliza nafasi ya tisa katika msimamo wa ligi kuu msimu uliopita ikiwa imecheza mechi 30 ilishinda michezo 11, ilitoka sare nne na kupoteza kupoteza michezo 15na kumaliza ikiwa na alama 37.
“Kwa sasa tunaipitia ripoti ya kocha na baada ya hapo tutaanza usajili kwa ajili ya msimu ujao, tunataka kusajili mapema ili tuanze ‘pre season’ mapema, kwa sababu moja ya vitu vinavyoangusha vilabu vingi ni kuchelewa kuanza maandalizi ya msimu mpya, mipango yetu yote kwa ajili ya msimu ujao tutatoa taarifa rasmi hivi karibuni,”amesema kiongozi huyo.