Bernard Membe amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania Urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo huku akiweka wazi shauku ya kutaka mazungumzo na CHADEMA kuungana wapate mgombea mmoja.
Hatua ya Membe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani inakuja siku moja baada ya kupokelewa rasmi katika Chama hicho. Membe amehamia ACT baada ya kufukuzwa uanachama na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Membe amesema huu ni wakati muafaka kwake kushiriki katika mazungumzo na vyama vingine ikiwemo CHADEMA ili kusimamisha ‘kisiki cha mpingo’ kimoja.
Wakati hayo yakijiri , mtia nia wa Urais kupitia tiketi ya CHADEMA ambaye pia ni mwenyekiti wa kanda ya kati Lazaro Nyalandu amesema chama hicho kitaibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu kwakuwa kimetengeneza muunganiko mzuri baina ya mgombea Urais,Ubunge,Udiwani na wananchi.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kufanyika kwa mdahalo wa kuwachuja watia nia wa nafasi ya ubunge jimbo la Njombe mjini ambapo ametumia fursa hiyo pia kuomba udhamini kwa wajumbe ili kupeperusha bendera ya nafasi ya Urais Nyalandu amesema kwa kuwa Chadema kimezidi kufanya mambo yenye mvuto kwa umma wana imani kitaibuka kidedea katika nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu.
“Kama unagombea Udiwani,Ubunge naomba ujiandae kufanya kampeni tena ufanye kampeni kweli kweli kama unategemea utakuja kutangazwa unapoteza muda wako hata tangazwa mtu atatangazwa mshindi” amesema Nyalandu.