Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ametoa kauli yake ya kwanza baada ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfukuza uanachama, leo, Februari 28, 2020.
Kupitia ukurasa wa Twitter, Membe ameeleza kuwa amepokea taarifa za kufukuzwa kwake katika chama hicho na kwamba atazungumza muda sio mrefu na Watanzania.
“Watanzania wenzangu nimepata habari ya kufukuzwa kwangu kutoka kwenye Chama changu cha CCM. Simu zinamiminika hadi nashindwa kuzijibu. Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote muda si mrefu,” ameandika.
Kamati Kuu ya CCM imefanya maamuzi makubwa matatu leo. Kwanza imemfukuza Membe uanachama, pili imetoa kalipio kali kwa Katibu Mkuu wa zamani Abdulrahman Kinana na mwisho imemsamehe Katibu Mkuu wa zamani, Yusufu Makamba.
Akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu akiwa katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema kuwa Kamati ya Nidhamu pia imepewa siku saba kukamilisha taarifa yake na kuiwasilisha.
Membe alihojiwa jijini Dodoma huku Makamba na Kinana wakihojiwa jijini Dar es Salaam, wote walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya kinidhamu.
Uamuzi wa kuwahoji watatu hao ulitolewa na Halmashauri Kuu ya chama, Desemba 2019.