Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe, amesema kuwa kabla hajafukuzwa na chama chake cha awali Chama cha maoinduzi (CCM), alikuwa anao mpango wa kukipindua chama hicho kiuongozi kwa kushirikiana na watu wengine sita na alikuwa na jumla ya wabunge 78.
Membe ametoa kauli hiyo leo Oktoba, 19, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo pia ameeleza mustakabali wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 28 ,mwaka huu, kwa kuuaminisha umma wa Watanzania kuwa yeye ndiye mgombea urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo.
“Mimi nilikuwa CCM nikataka kukabiliana na rais aliyepo madarakani peke yangu kumuondoa, lakini washukuru walinifukuza, tulijianda na wana CCM wenzangu, achilia mbali tulikuwa watu 6 tuliokuwa tayari kuiondoa serikali madarakani, mimi nilikuwa na wabunge 78, kwa bahati mbaya 46 wamefyekwa lakini wako CCM, 32 wamebaki hata mkininyonga siwezi kuwataja kwa sababu watatumbuliwa tu”, amesimulia Membe.
Haya yanajiri wakati Viongozi wakuu wa Chama cha ACT- Wazalendo wakionekana kumuunga mkono mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Tundu Lissu.
“Sisi tupo wa moja waliosema ni individuals (watu binafsi) na tumeyamaliza, chama cha ACT tuna mgombea, na ni mimi. Wapo watu ndani ya Chadema hawatampigia Lissu kwa hiyo hata Zitto na Maalim ni ACT lakini wanaweza wasinipigie kura ila tunaamini watabadilisha maamuzi yao ila tupo pamoja.”
Kwa mujibu wa Membe, nadharia kwamba wapinzani wakiungana wanaweza kukiangusha chama tawala haijawahi kufanikiwa Afrika, japo kwa Tanzania anaamini wamefanikiwa kuleta mpasuko kwenye chama tawala CCM.