Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP nchini Tanzania, Dkt Reginald Mengi amesema kuwa sababu kubwa ya yeye iliyomsukuma mpaka kufikia hatua ya kuandika kitabu kinachoelezea maisha yake kiujumla ni kutokana na mtoto wake Roodney ambaye ameshafariki kumsisitizia kuandika kitabu.
Mengi ameyasema hayo wakati alipokuwa anazungumza mbele ya wageni na viongozi wa nchi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa kitabu chake kilichopewa jina la ‘I Can, I Must, I Will- The Spirit of Success’ iliyofanyikia katika ukumbi wa Serena Hotel Jijini Dar es Salaam.
“Nilikuwa na mtoto Roodney lakini kabla hajaondoka hapa duniani aliniomba sana niandike kitabu ambacho kitacho kuwa kinaelezea maisha yangu na mambo ambayo nimeyafanya kwa hiyo nimefanya hivyo kama alivyotaka mwanangu na leo namshukuru Mungu nimeweza kutimiza ahadi yangu,“ amesema Dkt. Mengi.
Aidha, mbali na hilo Dkt. Mengi amesema jambo kubwa lililoweza kumsukuma mpaka kuzindua kitabu chake hicho ni kutokana na yeye kuzaliwa katika maisha ya kimasikini kitu ambalo ametaka wananchi wafahamu hilo ili nao waweze kujua namna ya kutoka huko na kuwa katika maisha mengine.
Hata hivyo, kwa upande wake, Rais Dkt. John Magufuli ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo ya uzinduzi wa kitabu cha ‘I Can, I Must, I Will- The Spirit of Success’ amewataka watanzania na wafanyabiashara wote kiujumla kununua kitabu hicho ili kiweze kuwafundisha katika kutokana na hali ya umasikini huku akiwasisitizia zaidi kufanya kazi kwa bidii na kuacha kusikiliza maneno ya watu ambao wanawakatisha tamaa.