Msanii maarufu , Menina Abdulkarimu Atiki ambaye pia ni mshereheshaji, ameipandisha kizimbani kampuni ya utengenezaji wa maudhui ya runinga kupitia ving’amuzi vya DSTV, MultiChoice South Africa na mshirika wake nchini, MultiChoice Tanzania akiidai fidia ya kiasi cha pesa kisichopungua Shilingi 1.12 bilioni kwa madai ya kumkashifu kupitia maudhui waliyorusha.
Wengine katika kesi hiyo wametajwa kuwa ni pamoja na mhariri wa kipindi cha ICU- Chumba cha Umbea kupitia channel ya Maisha Magic Bongo kilicho chini ya MaultiChoice Tanzania na Watangazaji wa kipindi hicho ambao ni Maimartha Jesse, Juma Lokole na Kwisa Thompson.
Katika kesi hiyo inayotarajiwa kusikilizwa tena Novemba 10,2021, Menina anadai Juma na wenzake walimchafua katika kipindi chao kinachorushwa kwenye chaneli ya Maisha Magic Bongo wakisema kuwa Menina hakuwa anampenda mume wake ambaye kwa sasa ni marehemu na kwamba hakuwa na maadili kama mke ndani ya nyumba.
Menina amedai kuwa kipindi hicho kimeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zake za ubalozi wa bidhaa, muziki, filamu na ushereheshaji ambazo zinahitaji kudumisha sifa njema kulinda jina na heshima na kwamba itamchukua takribani miaka mitano kusafisha jina na heshima yake, hivyo ataathirika kwa kupoteza kipato kikubwa ambacho amekuwa akikipata kwa shughuli hizo