Mabingwa wa Tanzania bara Young Africans wamevuna matunda ya malumbano badala ya maandalizi kufuatia kufungwa bao 1-0 na TP Mazembe ya DRC katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo kwa Young Africans, baada ya Juni 19 kufungwa pia 1-0 na wenyeji MO Bejaia 1-0 nchini Algeria.

Shujaa wa Mazembe leo alikuwa ni Mereveille Boppe aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Chrtistian Luyindama dakika ya 74.

Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure, Mazembe walionyesha kiwango kikubwa zaidi ya Young Africans kuashiria kwamba walistahili ushin di huo.Pamoja na ubora wa Mazembe, lakini leo Young Africans ilicheza chini ya kiwango, wachezaji wake wakionekana kabisa kucheza kwa woga na kutojiamini.

Shambulizi la maana la Young Africans lilikuja dakika ya 44 tu baada ya mshambuliaji Mzimbabwe kufanikiwa kumzidi mbio na maarifa beki Luyindama na kumpasia kiungo Deus Kaseke aliyepiga nje akiwa amebaki na kipa, Sylvain Gbohouo Guelassiognon.

Kipindi cha pili, Mazembe walifunguka zaidi na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Young Africans hadi kupata bao lao pekee.

Kiungo Mzambia, Obrey Chirwa hakuwa na madhara leo, wakati kiungo chipukizi mzalendo Juma Mahadhi alijitahidi ingawa hakuweza kumaliza mechi baada ya kuumia na kumpisha Geoffrey Mwashiuya dakika ya 69.

Kuelekea mchezo huo, Young Africans walitumia muda mrefu kulumbana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya matangazo ya Televisheni hadi wakaamua kufuta viingilio siku mbili kabla ya mechi.

Young Africans watahitimisha mechi zake za mzunguko wa kwanza za Kundi A kwa kucheza na Medeama ya Ghana Agosti 7 Uwanja wa Taifa pia.

Vikosi kamili vya leo ni Young Africans; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Juma Mahadhi/Geoffrey Mwashiuya dk69, Obrey Chirwa/Matheo Simon dk71 na Donald Ngoma.

TP Mazembe; Sylvain Gbohoud Guelassiognon, Jean Kasusula, Issama Mpeko, Salif Coulibaly, Rodger Asale, Adama Traore/Deogratius Kanda dk76, Merveille Bope, Nathan Sinkala, Koffi Christian/Jose Bodibake dk80, Christian Luyindama na Thomas Ulimwengu.

Uganda Kukomesha Mambukizi Mapya ya VVU kwa Watoto Wachanga 2017
Lesotho Kurejesha Viongozi wa Upinzani Nchini