Mshambuliaji wa kutegemewa wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi amesema kuwa imemuuma sana kukosa penati iliyosababisha kutoka sare ya 1-1 na Iceland kwenye mechi ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia.
Mkwaju wa penati wa Messi ambao ulivuta lenzi za macho ya wengi uliishia mikononi mwa mlinda mlango Hannes Halldorsson na kuzima matumaini ya Argentina kujitwalia alama tatu muhimu.
Messi anatazamwa akisaka kuifikia rekodi ya mshindani wake Cristiano Ronaldo ambaye alifanikiwa kupata ‘hat-trick’ kwenye mechi nzito kati ya Ureno na Uhispania, Ijumaa iliyopita.
“Kwa kawaida inauma sana kukosa penati. Kama wangefungua zaidi tungeweza kupata nafasi zaidi,” alisema Messi.
“Tuna uchungu wa kushindwa kuzipata alama tatu ambazo tulistahili. Kuanza na ushindi ni muhimu wakati wote, sasa tunatakiwa kuanza kufikiria kuhusu Croatia. Tutajaribu kulipita hili haraka,” aliongeza.
Alisema kuwa mbinu ya Iceland ilikuwa ngumu kwa upande wake kwakuwa wahakutaka kucheza sana bali walijikita katika kuziba lango lao.
Tayari Messi amekosa penati nne kati ya penati saba za mwisho alizowahi kupiga kwenye klabu yake ya Barcelona na timu yake ya taifa.
Croatia ambayo inasubiri kukutana na Argentina pamoja na Iceland, jana ilijitwalia alama 3 muhimu baada ya kuifunga Nigeria 2-0.
Magoli ya Croatia lilitokana na Oghenekaro Etebo kwa kujifunga (dakika ya 32) na Luca Modri (dakika ya 71) kwa mkwaju wa penati.