Mshambuliaji na nahodha wa mabingwa wa Hispania FC Barcelona Lionel Messi, huenda akarejea katika orodha ya wachezaji majeruhi wa klabu hiyo, kufuatia kuumia usiku wa kuamkia leo.
Messi alikua sehemu ya kikosi kilichoanza dhidi ya Villareal kwenye Uwanja wa Nou Camp, na ulikua mchezo wake wa kwanza kufanya hivyo tangu alipopona majeraha nyama za paja.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, aliumia mguu na inakua bahati mbaya kwake, kwani amekumbwa na mkasa huo, akiwa ametoka kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA.
Hata hivyo bila ya Messi, FC Barcelona walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja, yaliyofungwa na Antoine Griezmann na Arthur, huku bao la Villarreal lilifungwa na kiungo Santi Cazorla.
Meneja wa FC Barcelona, Ernesto Valverde alithibitisha kuumia kwa Messi mara baada ya mchezo huo, kwa kuwaambia waandishi wa habari kuwa, mshambuliaji huyo hakupata maumivu makubwa.
“Amepata maumivu kidogo, unajua tukio lolote linalompata Messi kila mmoja analipokea kwa mshtuko mkubwa, tutaangalia afya yake,”alisema Valverde.
Michezo mingine ya ligi kuu ya Hispania iliyochezwa usiku wa kuamkia leo.
Granada 1-1 Real Valladolid
Real Betis 1-1 Levante.