Kiungo wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil amejisifia kwa kuonyesha soka safi usiku wa kuamkia leo, wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Leicester City, waliokubali bakora tatu kwa moja, kwenye uwanja wa Emirates jijini London.
Ozil ambaye jana alikua nahodha wa kikosi cha The Gunners, alionyesha kandanda safi huku akifunga la kusawazisha dakika ya 44, baada ya Leicester City kuongoza kwa bao la kujifunga lililosababishwa na beki wa pembeni Héctor Bellerín dakika ya 31.
Kiungo huyo kutoka nchini ujetrumani amejimwagia sifa kupitia ukarasa wake wa Twitter kwa kuandika “Soka la kuvutia “.
Mbali na kujisifia katika mtandao wa Twitter, meneja wa Arsenal Unai Emery pia alikaririwa na vyombo vya habari akisema, hana budi kumpongeza kiungo huyo kwa juhudi na maarifa makubwa laliyoyaonyesha kwenye mchezo huo.
“Kiwango kutoka kwa Mesut Ozil kilichoonekana leo (Jana), kilikua ni kiwango cha hali ya juu,” alisema meneja huyo kutoka nchini Hispania.
“Ninafikiri tunaweza kucheza vizuri zaidi ya hapa, endapo kila mmoja atawajibika vyema, tunapaswa kuendelea hivi ili kufanikisha furaha kwa mashabiki wetu.”
Mabao mengine ya Arsenal katika mchezo huo yalifungwa na mshambuliaji kutoka nchini Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya beki wa pembeni kutoka nchini Uswiz Stephan Lichtsteiner.
Mshambuliaji huyo aliifungia Arsenal bao la pili na la tatu dakika ya 63 na 66 akimalizia pasi za mwisho za Héctor Bellerín na Mesut Ozil.