Mkuu wa benchi la ufundi la Kagera Sugar, Meck Mexime ameziita mezani timu zote zinazohitaji huduma yake baada ya kuhusishwa kwa muda mrefu na tetesi za kuwa mbioni kujiunga na Young Africans.
Mexime amesema hatajali sana hata kama atakuwa ni kocha msaidizi ataangalia maslahi yake kwakua ataendelea kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa kocha mkuu.
“Mimi ni kocha kazi yangu ni kufundisha mpira, sio Young Africans tu ambao ndio wanaotajwa tajwa timu yoyote itakayo nihitaji ije tu mezani tukubaliane.”
“Kuhusu kama nitakuwa kocha msaidizi au la hilo pia siliangalii sana. Hata kama nitakuwa msaidizi maana yake nitaendelea kujifunza mambo mbalimbali, na katika mpira nitaendelea kujifunza mpaka nitakapo staafu,” alisema Mexime.
Mwezi uliopita nahodha huyo wa zamani wa kikosi cha Mtibwa Sugar na timu ya taifa *Taifa Stars* alidai alishapewa mkataba na klabu ya Young Africans tangu mwishoni mwa mwaka jana, lakini kuna baadhi ya vipengele havikukaa sawa hivyo hakuusaini mkataba huo wala kuurudisha.
Inadaiwa kuwa mwenyekiti wa Young Africans, Dk. Mshindo Msolla ni shabiki mkubwa wa Mexime tangu anacheza nafasi ya ulinzi klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, na alikua mstari wa mbele kumpendekeza awe kocha msaidizi chini ya Kocha Mkuu Mbelgiji, Luc Eymael.