Meya wa Manispaa ya Temixco nchini Mexico aliyetajwa kwa jina la Gisela Mota Ocampo ameuawa kwa kupigwa risasi saa 24 baada ya kula kiapo na kukabidhiwa rasmi ofisi.

Duru kutoka nchini humo zimeeleza kuwa watu wenye silaha walivamia nyumbani kwake Jumamosi asubuhi (Januari 2, 2016) wakati familia yake ikiwa nyumbani hapo lakini walimuua yeye pekee.

Mwanasheria wa serikali wa Jimbo la Morelos  aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika tukio hilo, polisi walirushiana risasi na wavamizi hao na kufanikiwa kuwaua wawili kati yao. Alisema kuwa baadhi ya watu wazima na watoto wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio hilo na watafikishwa mahakamani.

Temixco inatajwa kuwa moja kati ya Manispaa zenye uhalifu wa jinai wa kiwango cha juu na maarufu kwa biashara haramu ya dawa za kulevya.

Serikali ya Morelos imetoa taarifa rasmi za kifo cha Mota Ocampo na kulielezea kama shambulizi lililoanzishwa na wahalifu dhidi ya katiba na demokrasia. Taarifa hiyo pia ilimuelezea Meya huyo kama mtu mwaminifu aliyekuwa amejitoa kwa taifa lake.

 

Zanzibar Ngoma Nzito, Serikali Yatangaza Bajeti ya Uchaguzi wa Marudio
Obama, Clinton Watuhumiwa Kulitengeneza Kundi la Kigaidi la ISIS