Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe (CHADEMA) amesema amepokea barua ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa inayomtaka aijibu ndani ya siku 5 juu ya tuhuma zinazomkabili ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.
Amesema, “Nimepokea barua ina tuhuma 4 ambazo ni matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya rasilimali za Halmashauri, mwenendo mbaya au ukosefu wa adabu na kushiriki katika vitendo vya rushwa.”
Amesema tuhuma hizo ni za kupangwa na hazina ukweli wowote na kuwa barua ya tuhuma hizo aliyoipokea haikuwa na majina ya Madiwani 19 waliotakiwa kuonekana wameunga mkono hoja tajwa.
Aidha, amesema “Kesho nitapeleka barua kwa Mkurugenzi nikimweleza na kuvikumbusha vyombo vya Usalama na watendaji wake taratibu na kanuni za kumtoa Meya madarakani wamezikosea”
Meya huyo ameeleza kuwa lengo la kupeleka barua hiyo ni kutaka kupewa nakala ya majina ya madiwani waliosaini hoja hiyo na kuomba ushahidi wa kila tuhuma ili ajibu.
Amesisitiza, “Nimekusudia kwenda Mahakamani kuzuia mchakato huu haramu wa kutaka kuniondoa madarakani, iwapo Mkurugenzi hatonipa majibu ya kuridhisha.”