Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita amezitaka halmashauri zote za jiji kuajiri watumishi ambao kazi yao kubwa itakuwa ni kuzika marehemu watakabainika kuwa hawana ndugu.
Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam wakati wa kikao cha robo ya pili ya Baraza la Madiwani wa jiji, ambapo amewaeleza madiwani hao kuwa jukumu la kuzika miili ya marehemu wasiokuwa na ndugu ni la halmashauri, hivyo wanapaswa kuwajibika nalo.
Amesema kuwa mpaka sasa jiji limeshanunua gari pamoja na vifaa mbalimbali vya kuhifadhia miili ya marehemu ambao wanakuwa hawana ndugu.
Aidha, Mwita amesema kuwa halmashauri ya jiji pamoja na halmashauri zingine zilizopo jijini humo walishakubaliana kuzika marehemu wasiokuwa na ndugu hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza makubaliano hayo.
“Mtakubaliana na mimi kwamba tulishaga kaa na kupeana majukumu kuhusu hili jambo, lakini mpaka sasa ni halmashauri ya Kinondoni tu ndiyo iliyotekeleza, sasa ninaagiza halmashauri zingine za jiji hili kuajiri watu hao,”amesema Mwita
Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila halmashauri za jiji la Dar es salaam kuajiri watu hao haraka zaidi ili kila mmoja atimize majukumu kiufasaha zaidi.