Mfahamu Othman Masoud Othman Sharrif, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Othman Masoud Othman almaarufu kama Ochu, ni Mzanzibari mahiri kwenye ulingo wa masuala ya sheria na mikakati.
Ochu alizaliwa Kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, mwanzoni mwa miaka ya sitini.
Baba mzazi wa Masoud, Sheikh Masoud Bin Othman alikuwa moja ya walimu mahiri wa dini misikitini, madrasa na hususan katika Skuli ya Pandani ambako alifundisha Quran.
Othman alianza masomo yake ya msingi katika Shule ya Pandani ambapo alionyesha umahiri mkubwa darasani, akishika nafasi ya kwanza katika miaka yake yote na kuwaacha wanafunzi wenzake kwa mbali sana kiwastani.
Kama ilivyokuwa matarajio ya wengi na Othman mwenyewe, alifaulu vizuri mitihani yake ya michepuo na kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika Skuli ya Fidel Castro, Chake Chake, Kusini Pemba.
Othman alipata ufaulu wa daraja la kwanza (Division One) na kufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa Shahada ya Kwanza katika Sheria (LLB).
Akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa mwanafunzi mahiri kwenye Kitivo cha Sheria akiwa na uwezo mzuri darasani na kujenga hoja kwenye mijadala na alihitimu masomo yake chuoni hapo kwa kupata digrii ya kwanza ya Sheria yenye heshima (Cum Laude/With Honors).
Alirejea Zanzibar na kuajiriwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Wizara ya Katiba na Sheria kama Wakili wa Serikali. Hapo, Serikali ilimpa ufadhili kwenda Chuo Kikuu cha London kuongeza ujuzi kwa kuchukua Shahada ya Pili ya Sheria (LLM).
Alipohitimu alirerejea Zanzibar na baada ya muda mfupi akateuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utawala Bora na Sheria katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Tano, chini ya Dkt Salmin Amour.
Rais Amani Abeid Karume alipoingia madarakani alimteua kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Mashtaka Zanzibar.
Novemba 2010 mara baada ya Dkt Ali Mohamed Shein kuchaguliwa kuwa Rais wa 7 wa Zanzibar, alimteua Othman kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Moja ya kazi kubwa ya Othman katika cheo hicho kipya ilikuwa mapitio ya sheria mbalimbali za Zanzibar na Muungano na katika mchakato wa majadiliano ya mabadiliko ya katiba ya Tanzania alikuwa nyota iliyotoa mwanga hasa kwenye mijadala migumu na tata iliyohusu mambo mbalimbali.
Wakati wa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, alisimamia utetezi wa mambo yanayohusu Zanzibar, hata kufikia hatua ya kupishana na msimamo wa Serikali akipiga kura ya kusimamia alichoamini kuhusu muundo wa Serikali.
Kutokana na sakata hilo, Othman alivuliwa nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baada ya sakata hilo Othman aliamua kuingia kwenye siasa, akiamini ni njia nyengine ya kusimamia yale anayoyaamini ambapo alijiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na kuteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa Chama na Mshauri Maalum wa aliyekuwa Katibu Mkuu CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.
Akshikilia nafasi hiyo Othman aliamua kurudi tena darasani akijiunga na Chuo Kikuu cha Turin nchini Italia kusoma Shahada namba mbili ya Uzamili (Master) katika Sheria (LLM) na kuhitimu vizuri.
Wakati wa mfarakano ndani ya Chama cha CUF uliosababisha mgawanyiko wa kiitikadi ambao ulipelekea Maalim Seif Sharif Hamad na kundi lake kutimkia ACT Wazalendo, Othman naye aliamua kuungana na Maalim Seif.
Othman ni msomi, mtumishi mahiri wa umma aliyeiweka Zanzibar moyoni na ni mtu anayetegemewa sana na chama chake cha ACT Wazalendo katika siasa za Zanzibar kutokana uelewa wake wa eneo hilo.
Alikuwa karibu sana na viongozi wakuu wa chama hicho hasa Hayati Maalim Seif, Jussa na Mazrui na alikuwa mtu aliyepewa nafasi sana kusimama kama Mgombea Urais Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho iwapo Maalim Seif angestaafu.
Mbali na siasa, Othman anamiliki kampuni yake binafsi ya masuala ya sheria iliyopo eneo la Mombasa mjini Zanzibar wateja wake wakiwa ni watu binafsi na makampuni na amekuwa akitoa huduma kama mshauri mwelekezi katika mashirika mbalimbali ya Kimataifa nje ya nchi.
Tarehe 28 Februari 2021 Chama cha ACT Wazalendo kilipendekeza na kupitisha jina la Othman Masoud Othman Sharrif kuwa mrithi wa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nafasi iliyoachwa na Maalim Seif ambaye alifariki dunia Februari 17, 2021 akiwa na miaka 77.
Machi Mosi 2021, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi alimtangaza Othman kuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar kumrithi Hayati Maalim Seif Sharif Hamad na kuapishwa Machi 2, 2021.
Tunaamini ataendeleza msimamo wa Maalim Seif, wa kuhakikisha Wazanzibar wanabaki wamoja na amani inadumu wakati wote kwa ajili ya maendeleo ya kila Mzanzibar.