Na: Josefly Muhozi
Ule msemo wa wenyeji wa Pwani ya Afrika ya Mashariki, “mtoto wa nyoka ni nyoka” umepata maana zaidi nchini Nigeria. Taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika, ambapo kati ya raia zaidi ya milioni 206 wa Taifa hilo, nitakueleza simulizi la maisha ya raia mmoja aliyeubariki msemo huo.
Maisha yake yamejaa visa na mikasa… kutoka kuukwepa mlango wa jela, sasa anaingia kwenye lango la Ikulu ya Nigeria na kukalia kiti cha mtawala mkuu wa Taifa.
Ni Bola Ahmed Adekunle Tinubu, mtoto wa mwanamke wa shoka Abibatu Mogaji, aliyekuwa mfanyabiashara katika soko la jiji la Lagos, huyu mama unaweza kumuita Mchaga wa Lagos. Alifahamika kwa kuzisaka fedha kwa nguvu zote akiwa sokoni hadi akapewa uongozi wa soko la Lagos. Mama huyu alibarikiwa kumzaa mtoto wa kiume, Machi 29, 1952. Hata hivyo, tarehe ya kuzaliwa kwa mtoto huyu nayo ilikuja kuwa tatizo… nitakueleza.
Alihakikisha kuwa mwanaye anakwepa ile imani kuwa mahitaji muhimu ya binadamu ni chakula, mavazi na makazi… akahakikisha anabeba imani waliyoificha wazungu kuwa mahitaji muhimu ya binadamu ni fedha, mamlaka na heshima (Waingereza wanaita money, power and respect). Ukipata hivyo mengine yote yanakuwa ndani yake. Huyu Mama aliishi miaka 96, akimuona mwanaye anavyopata fedha hadi kuvishtua vyombo vya dola vya Marekani akiwa na umri mdogo. Baba yake alikuwa wapi? Hatujui, maana asiyetajwa ujue lake halikuwepo.
Kwa nguvu ya fedha ya huyu Mama, Bola Tinubu alipata nafasi ya kusoma nchini Marekani, katika Chuo cha Richard J. Daley College kilichoko Chicago na baadaye katika Chuo Kikuu cha Chicago State, alipohitimu shahada ya sayansi ya uhasibu (Bachelor of Science Degree in Accounting).
Hata hivyo, suala la umri wa Tinubu bado ni mjadala mkubwa nchini Nigeria, kwani mara kadhaa amewasilisha nyaraka ambazo zimekinzana. Mfano, mwaka 1999 aliwasilisha nyaraka kwenye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambazo zilidai amezaliwa mwaka 1954 badala ya 1952. Pia, majina ya shule za awali (msingi na sekondari) yalikuwa yanatofautiana katika nyaraka hizo. Mwaka 2022 alipoamua kuwania urais, aliwasilisha nyaraka zisizoonesha shule ya msingi wala sekondari. Aliona isiwe tabu, mkanganyiko wa shule za msingi wa nini wakati yeye ni msomi wa shahada.
Tukirejea kwenye maisha yake ya nyuma zaidi… baada ya kumaliza masomo yake nchini Marekani, Tinubu alirejea nchini Nigeria mwaka 1983. Hata hivyo, maisha yake akiwa nchini Marekani yalionesha kuwa ni mtu mwenye fedha nyingi sana kiasi cha kuvishtua vyombo vya dola nchini humo. Raia huyo wa Nigeria aliendelea kula bata, na wazungu wakaendelea kufuatilia mienendo ya bata lake… mwaka 1983 alirejea nchini Nigeria akiwa na fedha nyingi, kisha akapata nafasi ya kufanya kazi kwenye Kampuni ya Kimarekani iliyowekeza nchini humo kwenye sekta ya mafuta, Mobil Oil. Alifanya kazi kwa bidii na maarifa, wamarekani wakamkubali kuwa ni jembe… wakampa ukuu wa taasisi hiyo nchini Nigeria. Yaani akawa Bosi Mkuu wa Mobil Oil Nigeria.
Hata hivyo, Serikali ya Marekani ilikuwa inaendelea na uchunguzi wake kuhusu fedha alizokuwa anamiliki katika akaunti kadhaa nchini humo. Tinubu alifanyiwa uchunguzi, na mwaka 1993 mali zake zikakamatwa kwa madai kuwa alikuwa anajihusisha na uwakala wa wafanyabiashara wawili wa dawa za kulevya wa Chicago katika miaka ya 1990. Nyaraka zilizowasilishwa Mahakamani dhidi yake zilieleza kuhusu tuhuma hizo.
Inaelezwa kuwa Tinubu aliivaa kesi hiyo iliyokuwa inatishia kumfunga jela maisha au kifungo kirefu, akayamaliza na serikali. Inadaiwa kuwa alilipa kiasi cha Shilingi $460,000.
Hatua hiyo haikumpunguzia nguvu Tinubu kuendelea kufuata kile alichofundishwa na Mama yake, kusaka fedha, kisha Mamlaka, kisha Heshima. Baada ya kuzipatia fedha vizuri, sasa alianza safari ya kusaka mamlaka ya kiutawala, akiwa amezima jaribio la kumuweka jela kwa kutumia fedha. Dawa ya moto ni moto, tatizo la kifedha linatatuliwa na fedha.
Si unajua tena, wahenga wa kizanaki walisema “penye udhia penyeza rupia.” Tinubu alikuwa na rupia na akakutana na udhia… hilo likapita, akaendelea kusaka hitaji muhimu la pili (mamlaka au nguvu ya utawala).
Mwaka 1992 alijiunga rasmi na harakati za kisiasa, akajiunga na chama cha Social Democratic Party. Akaanza kwa kasi kwenye ulingo wa siasa, akachaguliwa kuwa mjumbe wa Seneti akiwakilisha jimbo la Lagos Magharibi.
Mwaka 1993, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa kiraia wa urais nchini Nigeria ambao ulijaa vitimbwi na malalamiko ya wizi wa kura. Juni 12, uchaguzi huo ulifutwa. Tinubu aliunda kundi la National Democratic Coalition lililobeba harakati za kushinikiza Moshood Abiola atangazwe kuwa mshindi wa kiti cha urais.
Hata hivyo, alikutana na mkono wa chuma, ambapo mwaka 1994, Afisa wa Jeshi, Sani Abacha aliipindua Serikali na kutawala nchi hiyo kijeshi. Tinubu alikimbia uhamishoni akikwepa kifo. Alirejea nchini humo mwaka 1998, baada ya Sani Abacha kufariki dunia.
Aliendeleza harakati za kisiasa, ambapo alishinda katika uchaguzi wa mwaka 1999 kuwa Gavana wa Lagos, nafasi ambayo ilimjenga kuwa mwanasiasa maarufu akipitia vipindi vingi vigumu, vya kukosolewa na kusifiwa.
Alipakwa tope mara kadhaa kwa kuanzisha harakati za kulifanya jiji la Lagos kuwa la kisasa na kukomesha uhalifu. Alipata kashfa nyingi za rushwa na ufisadi wa kutupwa. Lakini bado alisimama. Maana alikuwa anaendelea kulitafuta hitaji la pili la nguvu za kimamlaka.
Mwaka 2015, ‘alipigwa na kitu kizito’ kichwani. Kama unavyofahamu, vyombo vya habari vina nguvu ya kukujenga ukaonekana nusu mtu nusu muungu; na vina nguvu ya kukuboa hadi ukaonekana haufai hata kuvuta hewa.
Kutokana na jinsi alivyokuwa anapambana kujijenga kisiasa na kuwasaidia wananchi wa Lagos kwa sera mbalimbali huku akikutana na vizingiti vikubwa, lakini anatusua, alianza kuwa juu. Akazungumziwa kila kona, kwa mazuri na mabaya.
Waingereza wanasema “When you are at the top, you become a topic” kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba “unapokuwa juu, unakuwa mada ya kuzungumziwa.” Akawa mti wenye matunda, akapigwa mawe kwelikweli.
Kwa mfano, mwaka 2009, alitajwa katika kashfa nzito, akidaiwa kuwa alihusika katika utakatishaji fedha na wizi wa fedha za umma. Lakini Tume ya Makosa ya Fedha na Uchumi ilimsafisha baada ya kufanya uchunguzi. Mwaka huohuo, chama chake kilidai kuna njama za kutaka kumuua. Kikatoa taarifa polisi na kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kumhakikishia usalama.
Sasa, unakumbuka nilikugusia kuwa Tinubu aliwahi kuchunguzwa kwa kashfa ya kujihusisha na dawa za kulevya…!? Ikawa hivi, mwaka 2015, chombo cha habari maarufu nchini humo cha African Independent Television (AIT) kiliandaa na kurusha makala maalum ya video, iliyofahamika kwa jina la “The Lion of Bourdillon”, ambayo ilieleza kwa kina kuhusu tuhuma za Tinubu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwa wakala wa wafanyabiashara wawili wa Heroine, raia wa Nigeria.
Wafanyabiashara hao walitajwa kuwa ni Adegboyega Mueez Akande na Abiodun Agbele. Makala hiyo pia ilieleza kwa kina kuhusu tuhuma za rushwa na ufisadi, ikimuangushia jumba bovu Tinubu. Makala hiyo yenye urefu wa saa moja, ilimpaka tope zito, uchafu mwingi ulizungumzwa juu ya Tinubu tena kwa lugha ya picha na maelezo.
Hata hivyo, walijitokeza waandishi wengine maarufu ambao waliikosoa vikali makala hiyo, akiwemo mwandishi nguli wa kike, Abimbola Adelakun. Yeye aliachia andiko lake Machi 5, 2015 akiikosoa vikali makala hiyo na kueleza kuwa ilifadhiliwa na wapinzani wa Tinubu ili kumchafua.
Lakini pia, Tinubu aliona pigo hilo lingeweza kumteketeza kisia, aliamua kukimbilia Mahakamani, akafungua kesi akidai makala hiyo inamchafua kwa taarifa za uongo. Katika kesi hiyo, Tinubu alidai fidia ya N150 billion (Naira bilioni 150).
Aprili 1, 2015 Mahakama iliamuru makala hiyo isioneshwe tena hadi kesi hiyo itakaposikilizwa. Wakati kesi inaendelea kusikilizwa, pande zote mbili ziliamua kukubaliana nje ya Mahakama, na makala hiyo ikapotezwa kwenye uso wa umma.
Mwaka 2014, Tinubu alifanikisha jambo kubwa. Aliandaa jukwaa na kumkabidhi aliyekuwa afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Nigeria, Jenerali Muhammadu Buhari kugombea urais wa Nigeria. Buhari alikuwa amejaribu kuwania urais mara tatu mfululizo akashindwa.
Lakini mwaka huu, Tinubu alisaidia kuunganisha vyama vya upinzani na kumpa nafasi Buhari kugombea urais. Kupitia umoja huu, Buhari alishida akiweka historia kwa mara ya kwanza nchini humo, chama cha upinzani kumshinda rais aliyekuwa madarakani. Buhari alimshinda Rais Goodluck Jonathan kwa tofauti ya kura zaidi ya Milioni 2.5. Rais Jonathan akasema, “niliahidi kutakuwa na uchaguzi huru na wenye haki, ninasimamia maneno yangu.” Akamkabidhi urais Buhari.
Katika uchaguzi mwingine wa Mwaka 2019, Tinubu aliendelea kumuunga mkono Buhari ambaye alishinda tena kuiongoza Nigeria.
“Ukitaka kufika haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzako.” Tinubu aliubeba vizuri msemo huu, akamshika mkono Buhari mara mbili mfululizo, na sasa ikafika zamu yake kufika mbali. Alisubiri, akawatanguliza wenzake tangu mwaka 1992, akawashika mkono wenzake, hakuwahi kuwa hata mgombea mwenza wa urais… lakini alikuwa anasubiri muda tu wa kufika mbali. Subira ikavuta heri.
Tinubu, akiwa ndiye raia wa Nigeria aliyeshika nafasi ya ugavana wa Lagos kwa muda mrefu zaidi, akaingia kwenye kinyang’anyiro cha urais akiomba mikoba ya Rais Buhari aliyemsogeza kwenye kiti hicho mara mbili (2014 na 2019).
Hatimaye, Mwaka 2023, umekuwa mwaka wake… Machi 1, 2023 Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigeria ilimtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkubwa kati ya wagombea watatu. Tibubu akaongoza akiwa na kura 8,794,726 (milioni nane laki saba, tisini na nne elfu, mia saba na ishirini na sita). Mpinzani wake Atiku Abubakar alipata kura 6,984,520 (milioni sita laki tisa themanini na nne elfu, mia tano na ishirini); na Peter Obi alishika nafasi ya tatu akiwa na kura 6,101,533 (milioni sita laki moja na moja elfu, mia tano na thelathini na tatu.
Sasa, baada ya kukwepa mishale yote, Tinubu anatarajia kuapishwa Mei 29, 2023 kuwa Rais wa Nigeria, na kufanikisha kupata mahitaji yote matatu aliyofundishwa na Mama yake, yaani Fedha, Nguvu ya utawala na Heshima (Money, Power and Respect) akiwa na umri wa miaka 70. Sasa ataitwa Mheshimiwa Rais Bola Tinubu.
Nikukumbushe tu kuwa, Tinubu ni kiongozi wa jadi (Chifu), na tajiri anayekadiriwa kuwa na ukwasi wa takribani dola za kimarekani bilioni 30 ($32.7 billion), takribani trilioni 75. Hata hivyo, hakuna uthibitisho rasmi kuhusu ukwasi huu ambao umeripotiwa na vyombo vya habari mara kadhaa. Lakini cha msingi ufahamu tu kuwa ni mtu mwenye pesa nyingi kati ya wenye pesa barani Afrika.
‘Chawa’ wake wanamuita ‘Bosi wa Mabosi’ (Boss of the Bosses), aliyekwepa mishale mingi na lango la gereza, sasa anaingia lango la Ikulu.