Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Diana Edward Bundala maarufu Mfalme Zumaridi kwa kosa la usafirishaji haramu wa Binadamu na Unyonyaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani humo kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ramadhan Ng’anzi, SACP amesema Zumarisi alikamwata jana majira ya jioni nyumbani kwake eneo la mtaa wa Buguku, kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu wapatao 149.
Watu hao wametolewa na kusafirisha toka sehemu mbalimbali kisha kuwafungia nyumbani kwake ambapo alikuwa akiwatumikisha, kati yao wanaume 57, wanawake 92 na miongoni mwao wapo watoto 24, wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya 4-17, ambao wamekatizwa masomo kinyume na sheria.
kamanda Ng’azi amesema hata hivyo Mwanamamam huyo amekuwa akiwaaminisha kuwa yeye ni Mungu anayeponya, kufufua wafu na kutatua matatizo yao.
Awali tarehe 23.02.2022 polisi walipokea amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni iliyotaka kumkamata mzazi wa kike wa mtoto Samir Ally Abbas ayetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo baada ya kesi ya msingi kusikilizwa na katika utekelezaji wa amri hiyo Polisi walifika Nyumbani kwa Mtuhumiwa Dianna Edward Bundala ambapo ilidaiwa yupo mzazi wa kike wa mtoto huyo na mtoto aliyetakiwa kufikishwa mahakamni.
Aidha baada ya askari kufika eneo la tukio mtuhumiwa akiongoza wafuasi wake waliwashambulia askari na kuwazuia kufanya kazi yao, ndipo askari waliondoka eneo hilo kwa nia ya kuepusha kutumia nguvu ambayo ingeweza kuleta madhara.
“Tarehe 26.02.2022 Askari Polisi walirudi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na kufanikisha ukamataji kwa mujibu wa sheria, Upelelezi wa kina unaendelea ili kubaini kiini cha watu hao kukusanyika katika nyumba ya mtuhumiwa ambayo sio nyumba ya ibada wala sehemu rasmi ya kongamano.” Alisema kamanda Ng’azi.
Baada ya upelelezi kukamilishwa Mtuhumiwa pamoja na washirika wake katika kutenda kosa watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
“Ndugu waandishi wa habari, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea kutekeleza maelekezo ya Mwendesha Mashitaka Taifa (DPP) ya kuwaachia jumla ya watuhumiwa 36 wa makosa ya vitendo vya kujihusiha na Ugaidi ambao wamekidhi masharti ya dhamana na pia tutawaachia watakaokidhi Vigezo vya dhamana,” aliongeza kamanda Ng’azi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa baadhi ya watu kuacha kutumia mwanvuli wa dini kuwahadaa wananchi wawapo na matatizo ya kijamii hususani magonjwa na hali ngumu ya maisha na pia Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi ambao waliona viashiria vya kinyonyaji na kutoa taarifa Polisi.
Mwaka 2019 viongozi wa Umoja wa Makanisa (UMJM), jijini Mwanza, unaoundwa na Mabaraza matatu ya TEC, CCT na CPCT, uliitaka Serikali kuyapitia upya Makanisa ambayo usajili wake haueleweki, ili kuondoa sintofahamu kwa waumini wa madhehebu hayo.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa ni siku chache baada ya Kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Dkt. Philis Nyimbi, kufungia Kanisa la Mfalme Zumaridi lililopo eneo la Iseni jijini humo ambalo linadaiwa kuendesha Ibada zake kinyume cha sheria na Katiba ya nchi.