Boniface Mbilinyi (32) ambaye hivi karibuni alikamatwa na jeshi la polisi akitaka kusafirisha kiasi kikubwa cha Dola za Marekani kwenda nje ya nchi kinyume na utaratibu, amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kudanganya kiasi cha fedha alichokuwa akitaka kusafiri nacho.
Mbilinyi anadaiwa kutamka kuwa na kiasi cha Dola 40,000 wakati alikuwa na Dola 123,000. Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Awamu Mbagwa, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kuwa Januari 13, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi umekamilika na wapo tayari kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Baada ya kusomewa kesi inayomkabili, Hakimu Shaidi alisema kwa kuwa kiasi hicho cha fedha zipo mikononi kwa serikali, aliamuru mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua na kitambulisho na kwamba fedha hizo zitasimama kama bondi na kesi imeahirishwa hadi Februari 7, mwaka huu.