Mfanyabiashara Sita John mwenye umri wa miaka 45, mkazi wa mtaa wa Kipondoda wilayani Manyoni, ameuawa na watu wasijulikana baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kwenye goti la kushoto.

Kamanda Polisi Mkoa wa Singida ACP Stella Mutabihirwa, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mfanyabiashara huyo aliuza gari yake mnadani na kupewa mifugo na fedha taslimu, jambo lililopelekea watu hao kumfuatia bila yeye kujua, na alipofika nyumbani wakamvamia na kupora fedha na kumuua.

Naye mke wa marehemu amejeruhiwa kichwani kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na watuhumiwa walifanikiwa kutokomea kusikojulikana.

Aidha jeshi la Polisi limemkamata mtuhumiwa mmoja baada ya kupata maelezo kwa mmoja wa wanafamilia ya marehemu alipolielezea jeshi la polisi kuwa amemtambua mtu mmoja, hata hivyo upelelezi juu ya tukio hilo unaendelea ikiwa ni sambamba na mtuhumiwa aliyekamatwa ili kufahamu watu anaoshirikina nao katika matukio ya uwizi na mauaji.

Hali ya majeruhi inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, lakini pia mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabiziwa wanafamilia kwaajili ya mazishi.

Sambamba na hayo yote Jeshi la polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kuachana na vitendo vya kujitafutia mali kwa njia zisizo halali.

Wawekezaji kutoka Sweden na Norway kuja Tanzania
Bajeti ya utafiti Wizara ya kilimo yaongezeka