Mahakama moja katika kaunti ya Nyamira nchini Kenya, imemhukumu kifungo cha miaka 15 Jela binti wa miaka 25 baada ya kukutwa na hatia ya kumnyanyasa kijinsia mtoto wa bosi wake mwenye miaka miwili aliekua akimlea.
Mshtakiwa huyo, Martha Bosire, alihukumiwa baada ya kesi yake kusikilizwa mbele ya hakimu Simon Arome katika mahakama ya hakimu mkazi Keroke, akituhumiwa kutenda kosa hilo kati ya Novemba 14, 2021 na Disemba 9, 2021.
Mtuhumiwa huyo alikubali makosa na kusema kuwa alikua akimuingizia vidole sehemu za uke mtoto huyo wa bosi wake kwa siku tofauti tofauti na baadaye anatumia ‘Spirit’ kutibu makovu ambayo yametokana na shughuli hiyo na kumnunulia pipi mtoto ili asitoe taarifa kwa wazazi wake.
Katika kujitetea, binti huyo aliiambia mahakama kuwa amekubali makosa na aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu huku akiomba majadiliano kwa sababu hana wazazi na ana mtoto mdogo ambaye anamtegemea akiahidi kutorudia tena makosa hayo.
Upande wa mashitaka ulisema kuwa, bibi wa mtoto ndiye aligundua kuwa mtoto ana shida baada ya kumuangalia sehemu zake za siri na kukuta ana majeraha ambayo yanaonekana na kuamua kutoa taarifa polisi.
Mtoto huyo kwa sasa anahudumiwa katika hospitali ya Borabu na hali yake inaendelea vizuri ambapo aligundulika kuwa na majeraha ya kingono.
Hata hivyo mfanyakazi huyo aliwapa mshituko watu wote waliokua mahakamani hapo baada ya kukiri mashitaka kwa haraka na kukubali hukumu bila kutetereka wakati alipokuwa akipelekwa jela kuanza kifungo chake.