Mvua zinazoendelea kunyesha katika safu za Milima iliyoko mikoa ya Arusha, Manyara na Kiteto zimesababisha kufungwa kwa daraja la Feri Dumila Mkoani Morogoro na kusababisha adha kwa wasafiri wa barabara kuu ya Morogoro – Dodoma.
Mvua hizo zimesababisha mafuriko na maji kuzingira daraja hilo hali iliyosababisha jeshi la polisi kwa kushirikiana na watendaji wa TANROADS kufunga barabara hiyo na kuzuia magari yoyote yanayokatiza eneo hilo la barabara.
Kazi inayofanywa kwa sasa na askari ambao wapo eneo hilo ni kuwazuia watu kuzingira eneo hilo na kuwataka abiria kuondoka katika eneo lote la daraja la Feri ili kuepusha madhara ikiwa daraja hilo litasombwa na maji.
Pamoja na madhara hayo kwenye barabara kuu, madhara pia yametokea kwa wananchi wa Kijiji cha Magore ambao wamekuwa wakilima pembezoni mwa mto huo unaomwaga maji yake hadi Mto Dakawa wamelalamikia kuharibiwa kwa mazao yao ikiwemo mahindi, bamia na nyanya chungu bidhaa ambazo zimekuwa maarufu kwa biashara katika eneo hilo.
Abiria na watumiaji wengine wa barabara hiyo wameombwa kuwa watulivu wakati jeshi la Polisi na TANROADS wakisubiri maji yapungue kufanya tathmini na baadae kuweza kuruhusu magari kuweza kupita.