Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, linamshikilia mfanyakazi wa ndani ambaye jina lake limehifadhiwa, kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuua mtoto wa bosi wake, aliyejulikana kwa jina la Tifan Osward, kwa kumnyonga shingo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda Masejo leo Juni 21, 2021, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 19 mwaka huu saa 12 jioni, katika eneo la Olasiti, jijini Arusha.

“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa binti huyo aliajiriwa miezi miwili iliyopita akitokea mkoa wa Mara, Jeshi la Polisi linaendelea kufanya upelelezi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

“Mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi ili kufahamu chanzo cha maamuzi hayo na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa uamuzi wa kisheria,” amesema Kamanda Masejo.

Rais Samia afanya mazungumzo na Rais Xi Jinping
LHRC waingilia kati swala la mtoto aliyeungua moto