Mwanamke mmoja mwananchi wa Uganda, aliyekuwa akifanya kazi za nyumbani nchini Saudi Arabia, amethibitika kuondolewa figo yake ya kulia na kwa mpango maalumu na mwajiri wake
Wizara ya mambo ya ndani nchini Uganda imethibitisha hilo, baada ya kupewa ripoti ya uchunguzi kutoka Hospitali kuu ya kitaifa ya Mulago na kuthibitisha kuwa sio ajali ya gari kama ilivyoarifiwa awali na mwajiri wake.
Mwanamke huyo, Judith Nakintu mwenye umri wa miaka 38 ana watoto watano na alichukuliwa na kampuni ya Nile Treasure Gate mnamo mwaka 2019 kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za nyumbani huko Jeddah nchini Saudi Arabia.
Baada ya kufanya kazi karibu miezi miwili, mawasiliano yake na familia yake yalikatika, ndipo mama yake mzazi alipoanza kufuatilia karibu miezi mitatu ndipo akaambiwa mwanae amepata ajali.
“Alitufahamisha kwa simu kwamba alipata ajali nilikuwa nataka kufahamu familia yake, nikamuuuliza alipata ajali bila kampuni iliyompeleka kujua? Nikawapigia simu kampuni yake nikawaeleza, wakasema hawana habari wala taarifa,” alisema mama huyo.
Kampuni ya Nile Treasure Gate ilimpigia mama wa Nakintu simu mnamo tarehe 30 Oktoba 2021. Mwanae alikuwa anatarajia kuwasili katika uwanja wa ndege wa Entebe siku hiyo. Aliondoka mpaka kwenye uwanja huo wa ndege kwa ajili ya kumpokea mwanae.
Alipowasili alimuona mwanae akiletwa kutoka kwenye ndege akiwa kwenye kiti cha wagonjwa cha magurudumu, hawezi kutembea na kuingizwa kwene gari la wagonjwa hadi Hospitali kuu ya Mulago na Kesho yake wakaruhusiwa kwenda nyumbani, lakini yeye hakuamini ripoti aliyopewa.
“Tulipolala hospitali maafisa wa kampuni waliyomchukua wakamleta daktari kufanya uchunguzi wa wa kitabibu wakasema yupo sawa hana tatizo, mimi sikuridhishwa, siku ya Jumatatu nikarudi Mulago wakamfanyia uchugnuzi upya nikaambiwa figo moja imetolewa,” alisema mama huyo.
Afisa mratibu wa kuzuia ulanguzi wa binadamu kutoka Idara ya Uhamiaji Uganda, Agness Igoye, amewaeleza waandishi wa habari kwamba, Hospitali kuu ya Mulago imethibitisha kwamba alitolewa figo moja.
Uchunguzi wa madaktari nchini Uganda umethibitisha figo yake ya kulia ilitolewa , uchunguzi wa awali wa Polisi umetambua muajiri wake wa nchini Saudi Arabia kwa jina la Sadaffa Muhamed, alitoa ripoti bandia za kitabibu kuwadanganya wanafamilia ya muathiriwa. Zilionyesha sehemu zake zote za viungo zipo sawa wakati sio kweli.
Kufuatia taarifa hiyo ya uchunguzi familia ya mwanamke huyo inaiomba serikali kusimamia suala hilo hadi haki itakapopatikana.